Katibu Mkuu Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC) Padri Charles Kitima


Dar es Salaam. Baraza la Maaskofu la Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), limemuomba Rais Samia Suluhu Hassan, kutumia mamlaka aliyo nayo, kusitisha wasilisho la ridhio la mkataba wa bandari, huku pia wakitaka hatua kama hizo zichukuliwe Bunge kwa kufuta ridhio lao.

Akisoma tamko la Baraza hilo, Padri Charles Kitima, amesema TEC inaisihi Serikali kusikiliza maoni ya wananchi kuhusu mchakato huo, akidai Watanzania na baraza hilo, hawakubaliana na hatua ya bandari ya Dar es Salaam, kuwa chini ya kampuni moja ya DP-World.

“Maaskofu wamerejea katika vifunguu kadhaa vya Katiba ibara 8 inayoeleza mamlaka ya nchi yapo kwa wananchi, kama hawataki, hata kuwe na mazuri kiasi gani maaskofu wamesema kwa ajili ya umoja na amani ni vema wananchi kusikilizwa,” Padri Kitima ambaye ndiye Katibu Mkuu wa TEC, amesema na kuongeza;

“Kwa kifupi mkataba huu, unagawa wananchi na kuwashinikiza kufanya kitu wasichokitaka, ndio maana sasa hivi wengine wapo upande huu na wengine kule. Hii ni kuigawa jamii, maaskofu wanasema kwanini wananchi walazimishwe kukubali bandari iendeshwe na mtu mwingine.


“Kwa sababu anapewa sehemu nzuri yenye biashara kubwa ya bandari. Pia maaskofu wanasema sasa hivi kuna shinikizo la mabadiliko ya sheria nyingi ili mkataba huu upite, sasa kwanini utawala wa nchi usifuatwe,” amesema Padri Kitima.

TEC pia imebainisha kasoro 10 katika IGA, ikidai makubaliano hayo yana hatari kwa Taifa huku baadhi ya ibara zake zina matatizo yatakayosababisha nchi kutofikia uhuru wa kiuchumi.

Agosti 10 mwaka huu, Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya ilitoa uamuzi juu ya huo ikisema mkataba huo hauna tatizo hivyo pingamizi lililowekwa na walalamikaji halina mashiko.


Uamuzi huo ulitolewa na majaji watatu likiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, akishirikiana na Mustafa Ismail na Abdi Kagomba.

Madai yaliyotolewa uamuzi na mahakama hiyo ni pamoja na: Kama ibara ya 2, 4(2)... zinakiuka Ibara namba 1, 8 na 28(1) na (3) za Katiba ya nchi na pia kama IGA ni mkataba kwa muktadha wa Sheria ya Mikataba.

“Mahakama imekubali kuwa Dubai ina mamlaka ya kuingia mikataba kama hiyo. Walalamikaji hawajaeleza kama Dubai imezuiliwa kuingia mkataba wa ushirikiano wa uwekezaji kwani ni suala la ushahidi,”amesema Jaji Ndunguru.

Mkataba huo wenye ibara 31 ulisainiwa Oktoba 25, mwaka jana baina ya Serikali ya Tanzania na ile ya Dubai ili kuendeleza na kuboresha uendeshaji wa miundombinu ya kimkakati ya bandari pamoja na maeneo maalumu ya kiuchumi, maegesho ya utunzaji mizigo na maeneo ya kanda za kibiashara.

Akisoma tamko hilo leo Ijumaa Agosti 18, 2023; lililokuwa na ujumbe wa ‘sauti ya watu, sauti ya Mungu’ mbele ya wanahabari, Padre Kitima ameiomba Serikali kusikiliza maoni ya wananchi kuhusu mchakato huo, akidai Watanzania walio wengi na baraza hilo, hawakubaliani na hatua ya Bandari ya Dar es Salaam, kupewa mwekezaji mmoja.


Alipoulizwa TEC imetumia njia gani kujua wananchi walio wengi hawautaki mkataba wa IGA, Kitima amesema baraza hilo, linakaa na wananchi kupitia jumuiya ndogo ndogo 67,000, parokia 1,300 na wanakutana na vikundi mbalimbali, akisema wamewasikiliza wanapokutana katika mazingira mbalimbali.

Pia, amesema TEC wameigawanya Tanzania katika majimbo 34 ambapo kuna maaskofu wanaokaa na wananchi, akisema ndio maana katika tamko hilo wametumia Watanzania walio wengi na sio kufanya sensa.


“Kwa kifupi mkataba huu, unagawa wananchi na kuwashinikiza kufanya kitu wasichokitaka, ndiyo maana sasa hivi wengine wapo upande huu na wengine kule. Hii ni kuigawa jamii, Maaskofu wanasema kwanini wananchi walazimishwe kukubali bandari iendeshwe na mtu mwingine,” amehoji.

Padri Kitima amesema TEC inaona ni vyema Serikali ikaendelea kuwajengea uwezo wa kitaifa kwa sekta za umma na binafsi za Kitanzania kwa kuweka ubia na kampuni zenye ubobezi wa kiteknolojia kutoka maeneo mbalimbali duniani, sio ubia kutoa Taifa moja.


Amesema TEC imekuwa ikifuatilia kwa umakini mijadala, maoni, mapendekezo na vilio vya wananchi waliowengi kuhusu na kubaini hawautaki mkataba wa IGA unaompa mwekezaji wa nje mamlaka ya na haki ya kumiliki njia kuu za uchumi.

“Tumebaini kama nchi, tumeshawekeza na kuendeleza bandari, reli na bandari kavu na tunaziendesha wenyewe, hii ndio shauku ya wananchi ili kujenga uwezo wetu. Tumegundua mapungufu yetu katika uendeshaji wa bandari, lakini tuna uwezo wa kuendelea kujidhatiti kurekebisha changamoto hizo na njia za uchumi zikabaki kwetu,” amesema Kitima.


“Historia inatufundisha kupuuza sauti za wananchi kuhusu mikataba kwa siku za nyuma, kumeisababishia nchi hasara kubwa ya kiuchumi, ukosefu wa ajira na mapato ya kuendesha huduma muhimu za afya, maji na elimu. Tumetafakari kwa makini kuhusu mkataba na kubaini unachochoea mgawanyiko katika kupambana na ukiukwaji mkubwa utawala wa sheria,” amesema.

Katika tamko hilo lenye orodha ya maaskofu 37 wa TEC, Padre Kitima alidai ibara ya 2 (1) inahusu lengo la mkataba huo la kuweka utaratibu unaoibana Tanzania kisheria katika kuendeleza, kuboresha na kuendesha bandari zote za maziwa, bahari na maeneo maalumu ya uwekezaji na usafirishaji mizigo.


Aliongeza kuwa ibara ya 4 inayohusu wigo wa mahusiano na utekelezaji unaoitaka Tanzania kuwajibika kwa kuijulisha Dubai kila fursa ya uwekezaji inapojitokeza. Hata hivyo, Kitima alisema hatua hiyo inakinzana na baadhi ya sheria za nchi hasa ile ya ushindani na manunuzi.

“Ibara 5 ambayo DP-World imepewa haki ya kuendeleza, kusimamia na kuendeleza miradi peke yake, huku Tanzania ikibaki na wajibu wa kumwezesha furahia haki hiyo. Wakati Ibara ya inataka Serikali kuwajibika kutoa mamlaka yanayotakiwa na mwekezaji bila ucheleweshaji.


“Pia ibara ya 6 inaitaka Tanzania kuwajibika kuipatia DP-World vibali na vivutio vya kutekeleza miradi yake kama Serikali, hii inapingana na baadhi ya sheria za kiutaratibu. Ibara ya 8 inazungumzia haki ya kutumia ardhi ambapo mkataba utasababisha uvunjifu wa sheria za ardhi na zinazohusu masuala ya ardhi,” amesema Kitima.

Mbali na hilo, Kitima amedai Ibara ya 10 inazungumzia usiri wa mkataba huo unaozuia mamlaka zingine zikiwemo Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Bunge kufuatilia mikataba. Huku akidai ibara za 23 na 24 zinaeleza ugumu wa kujitoa kwenye mkataba.


Padre Kitima amesema TEC inasisitiza kuhusu ‘sauti ya watu ni sauti ya Mungu’ na kuitaka Serikali kuwasikiliza wananchi na kufanya uamuzi kadri wanavyotaka ili Serikali kujijenge heshima ya kuwa na usikivu kwa Watanzania.

“Tunawajibika kimaadili, tunaona ni jukumu la Serikali kusikiliza wananchi wanaotaka mkataba huu uvunjwe,kwa kuwa tumeonyesha kuwa Tanzania tumeshawekeza na kuendeleza bandari, reli na bandari za nchi kavu.

“Ni wajibu miradi hii tuendeshe Watanzania wenyewe huku tukikaribisha ubia tutakaoudhibiti, hiki ndicho wananchi wanakililia kusudi tujenge uwezo wa wenyewe. Kwa maelezo hayo sisi TEC hatuungi mkono mkabata huu,” amesema Kitima.