Akiuza vifaa vya simu katika duka dogo la wazi katika mji mkuu wa Gabon Libreville, Doles Gabriel anamwona kiongozi wa mapinduzi Jenerali Brice Oligui Ngeuma kama Musa ambaye ameliondoa taifa kwenye minyororo ya bosi wake wa zamani - Rais Ali Bongo.
"Musa alisoma katika nyumba ya Farao, lakini Mungu alimteua kuwakomboa watu wa Misri kutoka utumwani. Hiki ndicho kinachotokea katika nyumba ya Bongo," kijana huyo mwenye umri wa miaka 23 alisema.
Maoni yake yalionyesha furaha - na matumaini - ya watu wengi walioishi chini ya Bongo. Kwa mkono wa chuma, familia hiyo ilitawala Gabon yenye utajiri wa mafuta kwa miaka yote isipokuwa saba tangu ilipopata uhuru wake kutoka kwa Ufaransa 1960.
Omar Bongo alikua rais mwaka 1967, akasalia madarakani hadi kifo chake mwaka 2009. Mwanawe, Ali Bongo, alimrithi hadi Jenerali Ngeuma alipompindua mwezi uliopita.
Jenerali huyo mwenye umri wa miaka 48 - alizaliwa katika jimbo la kusini-mashariki la Haut-Ogooué, ngome ya familia ya Bongo. Wengine wanasema yeye ni binamu wa rais aliyepinduliwa, na kwamba aliandaa mapinduzi ya ili kuhifadhi nguvu ya familia ya Bongo.
Jenerali Nguema alikuwa karibu sana na Omar Bongo, na Ali Bongo - alimteua kuwa mkuu wa kikosi cha ulinzi wa rais, na kumweka kusimamia usalama wake mwenyewe.
Lakini muda mfupi baada ya Bongo kutangazwa mshindi wa uchaguzi wenye utata mwezi uliopita, Jenerali Nguema alichukua mamlaka kutoka kwa mtu ambaye alipaswa kumlinda. Na kusema Bongo hakupaswa kugombea tena uchaguzi huo.
Wanajeshi wakiwa na silaha zao wakati wa kuapishwa kwa rais wa mpito Gen Nguema
Watu wengi niliozungumza nao katika mitaa ya mji mkuu, Libreville, wanaonekana kuwa na imani na rais wa mpito.
Umati mkubwa wa watu ulimshangilia wakati wa kuapishwa kwake.
“Alisema anakwenda kufanya uchaguzi na tunatarajia kwa neema za Mungu akiwa na hofu ya Mungu atafanya uchaguzi wa kuaminika,” anasema Hellen Paul Mongala, alikwenda kushuhudia kuapishwa kwa Jenerali huyo.
Hata hivyo, hafla hiyo ilisusiwa na mgombeaji mkuu wa urais wa upinzani Ondo Ossa, ambaye alishikilia kuwa Bongo alimwibia uchaguzi na hivyo basi, anafaa kuapishwa kama rais.
Baadhi ya wanachama wa upinzani wana mashaka makubwa kuhusu mapinduzi hayo, lakini wanaogopa kutoa maoni yao kwa uhuru.
Wanasema kwamba ingawa Jenerali Nguema amewaachilia kutoka gerezani baadhi ya wanaharakati wa ngazi za juu wanaounga mkono demokrasia na wanaharakati wa vyama vya wafanyakazi, bado hajaonyesha ni lini utawala wa kiraia utarejeshwa.
Hofu yao kubwa ni kwamba ana mpango wa kung'ang'ania madaraka - na Gabon itabaki katika hali ile ile.
Jenerali Nguema kufikia sasa amechukua mbinu ya maridhiano kwa rais aliyeondolewa madarakani, akisema yuko huru kwenda nje ya nchi.
Hii ni tofauti na Niger ambapo Rais Mohamed Bazoum amekuwa akishikiliwa - akiwa na mkewe na mwanawe - na jeshi la serikali lililompindua.
Lakini Bongo hadi sasa amekataa ombi la kwenda nje ya nchi, akipendelea kubaki katika makazi yake ya kibinafsi huko Libreville - jambo ambalo Waziri Mkuu aliyeteuliwa hivi karibuni Raymond Ndong Sima alithibitisha hilo kwa BBC.
"Hana mpango wa kuondoka kwa sasa. Nafikiri atasubiri kidogo. Pengine anasubiri kuona kile kitakachofuata," Sima alisema, akiongeza kuwa "hakuna kizuizi kwa uhuru wake."
Watu wengi nchini Gabon wamekuwa wakimpigia kelele Jenerali Nguema kuhakikisha kuwa Bongo anashtakiwa kwa ufisadi, kwa madai kuwa rais aliyetimuliwa - na familia yake - wamejitajirisha kwa gharama ya taifa. Wanakanusha madai hayo.
Sima alitoa ishara zinazokinzana kuhusu iwapo Bongo atashtakiwa.
"Nadhani watu hawavutiwi kufungua kesi. Sidhani kama inawezekana kufungua kesi wakati huu," aliambia kipindi cha Newshour cha BBC wiki iliyopita.
Nilipomuuliza mimi iwapo Bongo na mawaziri wake wa zamani watafunguliwa mashtaka, alijibu: “Nafikiri hivyo. Mamlaka mpya tayari imetangaza kuwafungulia mashitaka wale wote waliohusika na ufisadi au utakatishaji fedha."
Hadi sasa jeshi hilo limewakamata watu watatu wa karibu wa Bongo kwa tuhuma tofauti zikiwemo za utakatishaji fedha, kusafirisha bangi na kughushi saini ya rais huyo wa zamani alipokuwa amepatwa na kiharusi.
Bw Sima alisema kuwa aliyekuwa mke wa Rais Sylvia Valentin Bongo - raia wa Ufaransa - pia anachunguzwa. "Anahojiwa kwa sasa na lazima ajieleze," alisema, bila kutoa maelezo ya tuhuma dhidi yake.
Gabon na Mkoloni Wake
Wagaboni wengi wamekulia wakijua utawala wa familia ya Bongo tu
Gabon ni nchi yenye utajiri wa mafuta, lakini thuluthi moja ya watu wake milioni 2.4 wanaishi chini ya mstari wa umaskini, kulingana na Umoja wa Mataifa.
Mchambuzi wa masuala ya fedha mwenye makao yake mjini Libreville na mwanasiasa wa upinzani Jean Gaspard alisema nchi hiyo ina uwezo mkubwa lakini sera mbovu zimefukarisha taifa hilo.
"Kampuni za kigeni zinazochimba mafuta nchini haziajiri wataalam wa Gabon lakini huleta wataalamu kutoka nje. Ni sekta za mafuta na mbao pekee ndizo zinazoendelezwa. Sekta nyingine hazijaendelezwa," anasema.
Gabon daima imekuwa ikidumisha uhusiano mkubwa na mkoloni wake wa zamani, Ufaransa, huku ushawishi wake ukionekana zaidi katika mji wa pwani wa Port Gentil, kitovu cha viwanda vya mafuta na mbao nchini humo.
Raia wengi wa Ufaransa wanaishi huko, na wanamiliki mikahawa na baa. Hisia za chuki dhidi ya Wafaransa ni kubwa mjini humo, huku baadhi ya biashara zinazomilikiwa na Ufaransa zikiteketezwa mwaka 2009. Hili lilipelekea Bongo kupiga marufuku maandamano ya kupinga Wafaransa.
Utawala wa kijeshi bado haujaeleza ikiwa itaondoa marufuku hiyo. Mwanaharakati wa kupinga Ufaransa huko Port Gentil, Kevin Moukadi, anasema anataka "Wafaransa waondoke Gabon."
"Tungependa kupata uungwaji mkono kutoka kwa mataifa mengine ya kigeni. Hatuwataki Wafaransa tena. Ni lazima waondoke katika nchi yetu ili tuwe huru," aliniambia.
Wanajeshi walionyakua mamlaka nchini Niger na pia Mali na Burkina Faso wamekuwa na chuki dhidi ya Ufaransa, wakiishutumu kwa kuendeleza udhibiti hata baada ya uhuru, lakini Sima anasema kuwa Gabon haitaiga mfano wao.
Ali Bongo na baba yake Omar Bongo, wameiongoza Gabon kwa zaidi ya miaka 40
Serikali ya kijeshi itadumisha uhusiano wake wa karibu na Ufaransa kwa kuwa ilikuwa mwekezaji mkuu nchini Gabon, huku pia itaimarisha uhusiano na mataifa mengine ili kukuza uchumi, Sima alisema.
"Zamani, hatukuwa na mahusiano mengi na nchi za Asia, lakini leo Wachina wamekuwa washirika wapya," aliongeza.
Lakini Sima aliweka wazi kuwa anathamini uhusiano na Ufaransa zaidi, akisema kuwa "ni nchi ambayo imetawala nchi yetu na ni nchi ambayo uhusiano wake ni wa zamani zaidi kwa hivyo inaeleweka huu ni uhusiano wenye nguvu."
Maoni yake ni ahueni kubwa kwa Ufaransa, ambayo imeshuhudia ushawishi wake ukipungua katika makoloni yake ya zamani barani Afrika katika miaka ya hivi karibuni.
Lakini ili kudumisha imani ya watu, serikali ya kijeshi italazimika kuboresha hali ya maisha - na kutimiza ahadi yake ya kufanya uchaguzi wa kuaminika.
Sima ana matumaini kwamba mabadiliko yatatokea.
"Mchakato unafanyika kwa utulivu. Kila kitu kinafanyika kwa amani. Hakuna fujo. Tunataka matokeo chanya kuelekea siku zijazo," alisema.




0 Comments