Rais Vladimir Putin amesema Jumatano kwamba wanasayansi wa Urusi walikuwa karibu kuunda chanjo ya saratani ambayo inaweza kupatikana kwa wagonjwa hivi karibuni.

Putin alisema katika mahojiano ya televisheni kwamba "tumekaribia sana kuundwa kwa kinachojulikana kama chanjo ya saratani na dawa za kinga za kizazi kipya".

"Ninatumai kwamba hivi karibuni zitatumika kwa ufanisi kama njia za matibabu ya mtu binafsi," aliongeza, akizungumza katika kongamano la Moscow juu ya teknolojia ya siku zijazo.

Putin hakutaja aina gani za saratani ambazo chanjo zilizopendekezwa zingelenga, wala jinsi gani.

Nchi na makampuni kadhaa zinafanyia kazi chanjo ya saratani.

Mwaka jana serikali ya Uingereza ilitia saini makubaliano na kampuni ya BioNTech yenye makao yake Ujerumani kuzindua majaribio ya kliniki yanayotoa "matibabu ya kibinafsi ya saratani", yanayolenga kufikia wagonjwa 10,000 ifikapo 2030.

Kampuni za dawa Moderna na Merck & Co zinatengeneza chanjo ya majaribio ya saratani ambayo uchunguzi wa hatua ya kati ulionyesha kupunguza uwezekano wa kurudia kupata saratani au kifo kutokana na melanoma - saratani hatari zaidi ya ngozi - kwa nusu baada ya miaka mitatu ya matibabu.