MOROGORO; POLISI mkoani Morogoro, imewatia mbaroni watu wanne kwa tuhuma kumtapeli kiasi cha Sh milioni 8.5 mfanyabiashara wa Kijiji cha Turiani, wilayani Mvomero, mkoani Morogoro baada ya kumuuzia vipande vya chuma akielezwa ni madini.

Kamanda wa Polisi Mkoa Morogoro, Alex Mkama amesema kuwa tukio hilo lilitokea Machi 28 eneo la Turiani na kwamba watuhumiwa wakitembea na gari maeneo mbalimbali na kufanya utapeli wa aina hiyo kwa wananchi hususani wafanyabiashara, wakiwaonesha vichuma hivyo vilivyopo kwenye vikasha wakiwaaminisha ni madini.

Amesema wa kwanza Hassan  Selemani (44), ambaye ni derive mkazi wa Dar es Salaam na wenzake watatu wakiwa na  gari ndogo aina ya Toyota Crown yenye namba za usajili T883 EER, walikuwa na vikasha vitatu vyenye vipande wa chuma vilivyowekwa kama madini walijipatia kiasi hicho cha fedha kutoka kwa mfanyabiashara wa masuala ya miamala ya fedha, ambaye jina lake limehifadhiwa.

Akielezea kwa undani, Kamanda Mkama amesema siku hiyo baada ya mnunuzi kubaini alichouziwa sio madini alienda kutoa taarifa Kituo cha  Polisi Turiani, ambao waliwasiliana na wezao wa Kituo cha Polisi Mvomero na kufanikiwa kukamata gari hilo kwa vile namba zake zilikuwa zinajulikana.