Ni mwaka mmoja sasa tangu mwanahabari wa Marekani Evan Gershkovich azuiliwe katika safari yake ya kuripoti nchini Urusi. Tumaini lake bora la kuachiliwa linaweza kuwa Vadim Krasikov, ambaye anazuiliwa katika jela ya Ujerumani, aliyehukumiwa kwa mauaji ambayo yaliamriwa na Kremlin.
Katika msimu wa joto wa 2013, mmiliki wa mgahawa wa Moscow alipigwa risasi katika mji mkuu wa Urusi. Mwanamume aliyevalia kofia aliruka kutoka kwenye baiskeli na kumpiga risasi mara mbili kabla ya kukimbia.
Miaka sita baadaye, kamanda wa Chechnya aliyekimbilia uhamishoni Zelimkhan Khangoshvili, aliuawa katika bustani ya Berlin yenye shughuli nyingi katika hali kama hiyo ya kutisha, akipigwa risasi na mtu aliyekuwa kwenye baiskeli kutumia bastola ya Glock 26 mchana peupe.
Mshambulizi huyo alikamatwa baada ya kutupa bastola na wigi kwenye mto Spree karibu na Reichstag, jengo la bunge la Ujerumani.
Pasipoti iliyo na jina "Vadim Sokolov" ilipatikana kwa muuaji wa Berlin, lakini viongozi waligundua haraka kuwa hilo halikuwa jina lake.
Mwanamume mwenye kipara, waliyemkamata alikuwa ni Vadim Krasikov, raia wa Urusi ambaye ana uhusiano na FSB, idara ya usalama ya Urusi - na mshukiwa mkuu wa mauaji ya 2013 huko Moscow.
Katika mahojiano ya hivi majuzi na mtangazaji wa Marekani Tucker Carlson, Rais wa Urusi Vladimir Putin alionekana kuthibitisha ripoti kwamba nchi yake ilikuwa inataka kuachiliwa kwa "mzalendo" Krasikov kubadilishana na mwandishi wa habari wa Marekani Evan Gershkovich.
Mwezi huu umetimia mwaka mmoja tangu Bw Gershkovich, ripota wa Wall Street Journal, kuzuiliwa nchini Urusi kwa tuhuma za ujasusi ambazo zinakanushwa na yeye, gazeti lake na serikali ya Marekani.
Bwana Gershkovich sio Mmarekani pekee katika jela ya Urusi ambaye hatima yake inaweza kuunganishwa na ya Krasikov. Mwanajeshi wa zamani wa Marekani Paul Whelan na raia wa Marekani-Urusi Alsu Kurmasheva pia wanazuiliwa nchini Urusi kwa mashtaka yanayotazamwa na wengi kuwa ya kisiasa.
Hata marehemu kiongozi wa upinzani wa Urusi Alexei Navalny, ambaye alikuwa akitumikia kifungo cha miaka 19 jela nchini Urusi, alisemekana kuwa sehemu ya mabadilishano yaliyohusisha Krasikov kabla ya kufariki, kulingana na washirika wake. Kufuatia uchaguzi wa Urusi, Rais Putin alisema amekubali kumwachilia Navalny ili kuachiliwa huru kwa " baadhi ya watu" wanaoshikiliwa na nchi za Magharibi, lakini Ikulu ya White House ilisema hiyo ndiyo mara ya kwanza kusikia juu ya makubaliano hayo.
Ikiwa gharama ya Rais Putin ya kuachiliwa kwa watu hao itaendelea kuwa hiyo, ina maana njia mwafaka zaidi ya kuachiliwa kwa Wamarekani waliozuiliwa itakuwa ni kubadilishana wafungwa kwa Krasikov inayohitaji ushirikiano wa Ujerumani, Marekani na Urusi.
Akizungumza na BBC, mwanasiasa wa Ujerumani Roderich Kiesewetter alisema makubaliano hayo yatalazimisha Berlin kuingia katika "diplomasia ya mateka". Kwa nini Putin anaonekana kutaka sana kumrudisha Krasikov?
Mauaji yaliyoidhinishwa na serikali
Vidokezo vya kwanza vya uwezekano wa mkono wa Kremlin katika mauaji ya Berlin vinatoka kwa historia ya Krasikov - au tuseme, ukosefu wa moja.
Hati zilizopatikana na tovuti ya uchunguzi ya Bellingcat zinaonyesha alikuwa akitafutwa kwa mauaji ya 2013 ya Moscow. Walakini, miaka miwili baadaye, hati ya kukamatwa iliondolewa na kitambulisho cha "Vadim Krasikov" kilionekana kutoweka.
Wakati huo "Vadim Sokolov", mwenye umri wa miaka 45, alionekana. Mnamo 2015 alipata pasipoti, na, mnamo 2019, nambari ya kitambulisho cha ushuru.
Mahakama ya Ujerumani ilihitimisha kwamba hati hii inaweza tu kuidhinishwa na Kremlin, na kwa hiyo kwamba Vadim Krasikov alikuwa na msaada wa serikali kwa mauaji ya Berlin.
"Mamlaka ya serikali ya Urusi iliamuru mshtakiwa kumuua mwathiriwa," hakimu kiongozi wa Ujerumani alisema baada ya kumhukumu Krasikov kifungo cha maisha gerezani .
Mwathiriwa wake, Zelimkhan Khangoshvili, alikuwa kamanda wa waasi wa Chechnya kati ya 2000 na 2004, wakati Chechnya ilikuwa inapigana vita vya uhuru dhidi ya Urusi.
Kwa waangalizi wa Magharibi, Bw Khangoshvili alionekana kuwa sehemu ya msururu wa mauaji yaliyoamriwa na Moscow ya watu waliotoroka Chechen kwenda huko Ulaya na Mashariki ya Kati.
Kremlin ilikanusha kupanga mauaji ya Berlin, na kutupilia mbali hukumu dhidi ya Krasikov kama "iliyochochewa kisiasa".
Hata hivyo, katika mahojiano yake na Tucker Carlson, Rais Putin alionekana kukiri pale aliposema mazungumzo yanaendelea kwa ajili ya mabadilishano yanayomhusisha "mzalendo" wa Urusi ambaye "aliyemwondoa jambazi" katika mji mkuu wa Ulaya.
Ulrich Lechte, ambaye yuko katika kamati ya maswala ya kigeni ya serikali ya Ujerumani, aliiambia BBC kwamba nia ya Rais Putin kumrejesha Krasikov "ni kukiri wazi kuwa na hatia na inaonyesha jinsi Urusi ilivyoweza kuchukua hatua katika nchi yetu kwa udhalimu na bila kupingwa".
Mkataba wa FSB na wauaji
Vadim Krasikov alikuwa wa kitengo cha siri cha 'Vympel' cha huduma ya siri ya Urusi, FSB, kulingana na waendesha mashtaka katika kesi yake.
"Majukumu yake rasmi ni operesheni za kukabiliana na ugaidi nyumbani, lakini kwa njia nyingi imerejea kwenye mizizi yake ya awali, kama kitengo kilichopewa jukumu la "kazi-nyevu" - hujuma na mauaji - nje ya nchi," anasema mwanahistoria wa Putin na mtaalamu wa usalama wa Urusi Mark Galeotti .
Krasikov binafsi alikutana na Putin kwenye safu ya kulenga shabaha alipokuwa akihudumu na Vympel, akimiliki BMW na Porsche, na alisafiri kwenda kazini mara kwa mara, kulingana na mahojiano ambayo shemeji yake alitoa The Insider.
Muungano kati ya Krasikov na FSB ungetoa maelezo ya kwa nini Vladimir Putin, afisa wa zamani wa ujasusi wa kigeni mwenyewe, atakuwa tayari kumkabidhi mfungwa wa thamani ya Evan Gershkovich.
Lakini Mark Galeotti alisema mpango unaowezekana unasema zaidi kuhusu mkataba wa kijamii wa Urusi na mawakala nje ya nchi kuliko thamani ya Krasikov kibinafsi.
"Ni [Urusi] inasema 'angalia, ikiwa utakamatwa, tutakurudisha nyumbani , kwa njia moja au nyingine. Inaweza kuchukua muda mrefu, lakini tutakurudisha'," Bw Galeotti alisema. "Hiyo ni muhimu sana kwa kuwafanya watu wajiweke katika hali zinazoweza kuwa hatari sana."
Lakini ikiwa Krasikov atawahi kuruhusiwa kurudi Urusi hatimaye ni juu ya serikali ya Ujerumani.
BBC iliwasiliana na wajumbe watatu wa kamati ya maswala ya kigeni ya serikali, ambao wote wanapinga kuachiliwa kwa Krasikov.
Ulrich Lechte, ambaye Chama chake cha Free Democratic ni sehemu ya serikali ya Kansela Olaf Scholz, alisisitiza kwamba Ujerumani "lazima isiifanyie Urusi neema hii".
"Hii ni aina ya msamaha na inatoa ishara ya kisiasa kwamba Urusi inaweza kutekeleza mauaji zaidi katika eneo letu, ambayo yataachiliwa na hivyo kubaki bila kuadhibiwa," Bw Lechte aliambia BBC.
"Lazima isikubaliwe kuwa raia wa kigeni wanakamatwa kiholela ili kuwanyanyasa kwa kubadilishana wafungwa."
Jürgen Hardt, kutoka chama cha Christian Democrats, alisema "hakuona uungwaji mkono wowote wa kisiasa" kwa ubadilishanaji wa uvumi unaomhusisha Krasikov.
Hata kama kulikuwa na dhamira ya kisiasa huko Berlin kumwachilia Krasikov, michakato ya kisheria ambayo inaweza kufanya hivyo inaleta changamoto zake.
Anaweza kusamehewa na rais, au kufukuzwa nchini ili kutumikia kifungo chake kilichosalia nchini Urusi - jambo ambalo bila shaka lisingetokea kwa kuzingatia maoni ya Putin.
Mfano mmoja ni wa mrusi anayefahamika kama the "Merchant of Death", Viktor Bout, mfanyabiashara maarufu wa silaha aliyeachiliwa kutoka chini ya ulinzi wa Marekani kama sehemu ya kubadilishana wafungwa na nyota wa mpira wa vikapu wa Marekani Brittney Griner. Bout sasa amejikita katika siasa na ameshinda kiti katika uchaguzi wa mitaa nchini Urusi.
Nicola Bier, wakili wa Ujerumani anayeangazia sheria ya kuwarudisha watu makwao, watu wanaozuiliwa na Urusi aliiambia BBC "hakuna utaratibu wa kisheria ambao umeundwa kwa hali hii", kwa hivyo hatua yoyote itakuwa ya utata na ya kisiasa.
Mwanaharakati wa kisiasa anayepinga Kremlin Bill Browder sasa anaandaa orodha ya zaidi ya wafungwa 50 wa Urusi katika nchi za Magharibi ambao wanaweza kutumika kama suluhu kuwaachilia wanaharakati na waandishi wa habari waliozuiliwa nchini Urusi.
Browder anatumai juhudi hizo zinaweza kusaidia kumwachilia mwanahabari wa Uingereza-Urusi Vladimir Kara-Murza, aliyehukumiwa kifungo cha miaka 25 jela kwa kosa la uhaini kwa kuzungumza dhidi ya vita vya Ukraine, pamoja na Evan Gershkovich.
Alipoulizwa na BBC kama kampeni yake ilihusisha "diplomasia ya mateka", Browder alikubali "Sio suluhu bora", lakini ni muhimu kuokoa maisha.
Baada ya kifo cha Alexei Navalny , Browder alisema, "ni wazi kwamba mateka wengine wako katika hatari ya kufa".
0 Comments