ARUSHA: Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Arusha limebainisha kuwa kikosi hicho kinaendelea na operesheni ya kuwakamata na kuwachukulia hatua wale wote ambao wamekaidi zoezi la kuondoa namba za 3D.

Kauli hiyo imetolewa leo na Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoani humo Mrakibu Mwandamizi wa Polisi SSP, Zauda Mohamed alipokutana  na viongozi wa madereva wa daladala mkoani humo kwa ajili ya kusikiliza changamoto zinazowakabili.

Mwenyekiti wa madereva daladala jijini Arusha, Albano Matemwe amesema sekta hiyo ya usafiri ilikua ikikabiliwa na changamoto nyingi, hivyo wakaona ni vyema kuomba kukutana na uongozi wa jeshi la polisi kuziwasilisha ili zipatiwe ufumbuzi.

Naye Godfrey Mlacha ambaye ni dereva daladala pamoja na mambo mengine, amesema kero kubwa wanayokutana nayo ni abiria kulazimisha kushushwa maeneo ambayo hayana vituo hali inayoibua migogoro baina yao.