DAR ES SALAAM: Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba ameshiriki Mkutano Maalum wa 22 wa Baraza la Mawaziri wa Umoja wa Afrika (AU) unaofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia leo, Machi 15, 2024.

Mkutano huo umepitia maandalizi ya mchakato wa uchaguzi wa uongozi wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika utakaofanyika mwezi Februari 2025 kwa nafasi za Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Kamisheni pamoja na nafasi sita za Makamishna wa sekta mbalimbali za AU.

Katika mjadala huo, Tanzania imesisitiza umuhimu wa uchaguzi wa nafasi ya Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti kuzingatia kanuni na taratibu za uchaguzi wa nafasi hizo ikiwemo uwazi, uwezo wa wagombea na usawa wa kijinsia.

Aidha, Tanzania imependekeza kufanyika kwa mjadala (Public Debate) kwa wagombea wa nafasi ya Mwenyekiti ili kutoa nafasi kwa wananchi wa Afrika kutambua maono ya wagombea watakaochaguliwa kuongoza Kamisheni ya AU.