IFAKARA, Morogoro: MKUU wa Wilaya ya Kilombero, mkoani Morogoro, Dunstan Kyobya amethibitisha kutokea kwa kifo cha mtu mmoja baada kutumbukia kwenye kina kirefu cha maji ikiwa ni madhara ya mvua kubwa iliyonyesha usiku wa kuamkia Machi 25, 2024.

Takribani kata nne za Halmashauri ya Mji Ifakara zimekumbwa na mafuriko hayo, hali inayopelekea wakazi wa kata hizo kufanya jitihada za kujinusuru na kunusuru maisha ya waathiriwa wenza wa mafuriko.

Wavuvi katika maeneo hayo wamelazimika kutumia mitumbwi kukatiza mijini kuokoa manusura ili kuwapeleka maeneo salama

Miongoni mwa kata zilizokumbwa na kadhia hiyo ya mafuriko ni kata ya Lumemo ambapo nyumba kadhaa zimejaa maji kutokana na mto Lumemo kufurika na maji yake kusambaa hadi kwenye makazi ya watu kati kati ya mji huo na kusababisha kuharibu vyakula vilivyohifadhiwa, kuharibu miundombinu ya barabara, madaraja, kuta za nyumba kadhaa kubomoka.