RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amezindua Duru ya Kwanza ya Utoaji wa Vitalu kwa Kampuni za Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia katika maeneo ya baharini Zanzibar.

Dk Mwinyi amesema serikali inakaribisha kampuni zote za utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi kushiriki katika duru hiyo.

Rais Mwinyi alihakikishia wawekezaji wa sekta hiyo kuwa serikali iko tayari kuhakikisha mazingira mazuri ya uwekezaji kwa manufaa ya wote.

Alisisitiza dhamira ya serikali katika kuimarisha uchumi wa buluu kwa lengo la kuharakisha maendeleo ya nchi na kuhakikisha upatikanaji endelevu wa vyanzo vya nishati ya uhakika.

Aidha, Rais Mwinyi alieleza kuwa uchumi wa buluu una fursa nyingi za kukuza mipango ya maendeleo ya kiuchumi yenye lengo la kupunguza umaskini na kujenga fursa za ajira nchini. Hatua hii inaonesha azma ya Serikali ya Zanzibar katika kutafuta njia mbadala za kukuza uchumi na kuleta maendeleo endelevu kwa wananchi wake.