DODOMA: WAKATI ripoti ya Takukuru ikibainisha Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kughushi nyaraka za fedha, ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imebaini madudu katika halmashauri 10 nchini.
Akiwasilisha ripoti hiyo leo Machi 28, 2024 Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa (Takukuru), CP Salum Hamduni amesema uchunguzi wao umebaini ubadhirifu wa Sh Bilioni 8.9 zilizokusanywa kwa njia ya mashine na halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.
“ Fedha hizo licha ya kukusanywa lakini hazikupelekwa benki, watuhumiwa walighushi nyaraka wakionesha fedha hizo zimepelekwa,”amesema CP Hamduni.
Kwa upande wa CAG Cherles Kichere amesema ukaguzi uliofanyika, amebaini halmashauri 10 zililipa kiasi cha Sh Bilioni 2.9 kwa kazi zilizotekelezwa bila kuwepo nyaraka zinazoonesha ukubwa wa kazi, wakati mamlaka nne zikilipa Sh Milioni 346.6 kwa kazi ambazo hazikutekelezwa kutokana na kukosekana usimamizi wa miradi.
Pia CAG Kichere amesema ukaguzi wake umebaini serikali imeingia hasara ya Sh.Bilioni 222.3 kwa kufanya matumizi yasiyokuwa na tija kwa kulipa faini kwa kuchelewesha malipo ya wakandarasi wanaojenga barabara.
0 Comments