Rais Joe Biden wa Marekani amemwambia Volodymyr Zelensky "atachukua hatua haraka" kutuma msaada mpya wa kijeshi wa Ukraine, baada ya wabunge wa Marekani kupitisha kifurushi cha msaada cha $61bn (£49bn).

Baraza la Wawakilishi liliidhinisha mswada huo siku ya Jumamosi baada ya miezi kadhaa ya msukosuko wa kisiasa katika bunge hilo.

Bw Biden aliahidi msaada "muhimu" kwa Kyiv - ikiwa ni pamoja na ulinzi zaidi wa anga - ikiwa maseneta wataidhinisha mswada huo kama ilivyotarajiwa Jumanne.

Uhakikisho huo unatokea wakati mashambulio ya Urusi yakiharibu mnara wa TV huko Kharkiv.

Picha zilionyesha mnara huo mwekundu na mweupe ukiporomoka sekunde chache baada ya makombora ya Urusi kuushambulia siku ya Jumatatu alasiri katika mji wa mashariki mwa Ukraine, ulio umbali wa maili 19 tu (kilomita 30) kutoka mpaka wa Urusi.

Maafisa wa eneo hilo walisema hakukuwa na majeruhi katika shambulio hilo, huku Gavana wa eneo hilo Oleg Syniehubov akiandika kwenye mitandao ya kijamii kwamba wafanyikazi walikuwa kwenye makazi wakati shambulizi hilo linatokea.

Bw Syniehubov aliongeza kuwa shambulio hilo limetatiza utangazaji wa televisheni katika eneo hilo.

Kharkiv imekuwa ikilengwa katika mashambulio ya angani yasiyokoma na vikosi vya Urusi katika wiki za hivi karibuni. Katika ujumbe mtandaoni baada ya shambulio hilo, Rais Zelensky aliandika kwamba ilikuwa "nia ya wazi ya Urusi kufanya mji huo usiwe na watu".

Aliongeza kuwa alikuwa amemjulisha Rais Biden kuhusu shambulizi hilo, ambalo alisema lilifanyika kabla ya kuzungumza kwa njia ya simu siku ya Jumatatu.