Katika mchezo maarufu wa kuigiza wa Romeo and Juliet ulioandikwa na William Shakespeare mnamo mwaka 1597, kuna sehemu Juliet alitamka maneno maarufu ya “What is in a name?”. Kufupisha hadithi ndefu, Juliet alisema waridi litabaki kunukia tu hata kama lingeitwa kwa jina lingine.

Baada ya Serikali ya Tanzania kutangaza kwamba kuanzia leo, Aprili 12, 2024, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Tanzania (NEC) itaanza kujulikana kwa jina jipya la Tume Huru ya Uchaguzi ya Tanzania, maoni ya wanasiasa wa vyama vya upinzani na wadau wengine yalinikumbusha mchezo ule wa kuigiza wa Shakespeare uliotungwa mwishoni mwa karne ya 16.

Chama cha ACT Wazalendo kupitia kwa viongozi wake wa juu wametoa matamshi hadharani ya kusema jambo la msingi kabisa si kubadili jina la tume hiyo bali kufuata matakwa ya sheria mpya ya Tume ya Uchaguzi ya mwaka 2024 iliyobadili jina la tume.

Chama kikuu cha upinzani na maarufu zaidi nchini Tanzania cha CHADEMA, kupitia kwa Katibu Mkuu wake, John Mnyika, kimeendelea na msimamo wake wa kutokubaliana na kuundwa kwa tume hiyo pasipo kwanza kufanya mabadiliko ya Katiba ya Tanzania.

Ni kama vile CHADEMA na ACT Wazalendo wanakubaliana na Shakespeare kwamba jina pekee la tume ya uchaguzi halifanyi tume hiyo kutimiza majukumu yake ipasavyo. Tume inaweza kuitwa huru na isiwe huru na inaweza isiitwe huru lakini ikawa huru.

Ingawa kwenye hilo ACT na CHADEMA wanakubaliana, lakini vyama hivyo na chama tawala cha CCM vinaonekana haviko njia moja kwenye suala zima la sheria tatu mpya za uchaguzi zilizosainiwa na Rais Samia Suluhu Hassan Machi 29. Sheria hizo ni Sheria ya Uchaguzi wa Wabunge na Madiwani, Sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria ya Tume ya Uchaguzi – zote za mwaka 2024.

CCM, ACT na CHADEMA katika hali tofauti

Tangu kuanza kwa mjadala na hatimaye kupitishwa kwa sheria hizo tatu, ni rahisi kuona njia tatu ambazo vyama vikuu vya siasa vya Tanzania vinaona mchakato huo. Kwa chama tawala, ni Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana pekee ndiye amezungumza hadharani kuunga mkono sheria hizo.

Kimsingi, baadhi ya waandishi wa habari wa Tanzania wamejikuta katika hali ngumu kupata maoni ya baadhi ya wabunge na wanasiasa wa chama tawala kuhusu maoni yao kuhusu sheria hizo. Ni kama vile wapo wanaoamini sheria hizo hazina faida kwao kama chama tawala.

ACT Wazalendo wanaonekana kuunga mkono sheria hizio mpya kwa sababu wao – pengine kuliko chama kingine chochote cha upinzani nchini, wameshiriki kuanzia hatua ya kwanza ya kutaka kufanyiwa mabadiliko ya sheria za uchaguzi kupitia Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) na kwenye Kikosi Kazi cha Rais Samia.

Mafanikio ya aina yoyote kwenye mabadiliko ya ufanyikaji na uendeshaji wa siasa Tanzania kupitia mchakato uliofanyika – kwa namna zote, yanaonekana kama ni mafanikio kwa ACT Wazalendo.

Kwa upande mwingine, CHADEMA haikuwa sehemu na haikuunga mkono mchakato uliofanikisha kupitishwa kwa sheria hizi. Tangu awali, msimamo wake ni kuwa kinachotakiwa ni mabadiliko ya Katiba ya Tanzania na si sheria zinazosimamia uchaguzi pekee.

Kwa CHADEMA – kuondoa ukweli wa madai yao ya Katiba, inatambua pia kwamba mafanikio ya mchakato uliofanikisha sheria hizi, yanakipa nguvu chama cha ACT Wazalendo na ushawishi wake na kwa sababu hiyo ni muhimu kwake kuendelea kupinga mchakato wenyewe na matokeo yake.

Kuhusu uhuru wa tume za uchaguzi

H

Kila ninapofanya uchambuzi kuhusu uhuru au uhalali wa Tume za Uchaguzi barani Afrika, kigezo changu kikubwa huwa ni andiko maarufu la kisomi la mwaka 2020 la maprofesa wawili; Nic Cheeseman na Jorgen Elklit – Understanding and Assessing Electoral Commission Independence: A New Framework. (Uelewa na tahmini ya uhuru wa tume ya uchaguzi: Mwelekeo mpya) Wasomi hawa walitoa vigezo vitatu vya kueleza endapo tume ni huru au si huru.

Vigezo hivyo ni; Utaasisi wa tume, namna inavyofanya kazi zake na uwezo wake kibajeti. Kwenye eneo la utaasisi wa tume inazungumzia ilivyoundwa kisheria, aina ya watu wanaoiongoza na weledi wao. Kwa vigezo vya akina Cheeseman, tume haiwezi kuwa huru kwa kubadilishwa jina pekee. Uhuru ni utaasisi wake, weledi wa watumishi na wajumbe wake na kuaminika kwake mbele ya jamii.

Inafikirisha kwamba katika andiko hilo la maprofesa hawa – mmoja wa demokrasia na mwingine wa sayansi ya siasa, kuna mahali wameandika kwamba tume nyingi za uchaguzi zinazoitwa huru, kiukweli hazina uhuru isipokuwa ni jina tu.

Hoja kuu ya Kiongozi wa Chama wa ACT Wazalendo, Dorothy Semu, ni kuwa ingawa tume sasa itaitwa huru, wajumbe wake ni walewale wa zamani na hivyo wanatakiwa kuchaguliwa wengine watakaoendana na “roho” ya sheria mpya.

Kwa mujibu wa sheria mpya, wajumbe wapya wanatakiwa kuomba nafasi hiyo na kupitishwa na Tume ya Usaili. Wajumbe wote waliopo sasa walipata nafasi hizo kwa uteuzi wa Rais wa Tanzania kwa mujibu wa matakwa ya sheria iliyokuwepo awali.

Muktadha wa tume za uchaguzi za Afrika

Kufananisha uhuru na utendaji wa tume za uchaguzi za Afrika ni jambo lenye changamoto. Tume Huru ya Uchaguzi ya Kenya ilikuja baada ya mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2010. Hata hivyo, utafiti wa akina Cheeseman ulionesha nayo haikuwa “huru” kama neno lenyewe lilivyo.

Tume ya Uchaguzi ya Afrika Kusini ni miongoni mwa zinazosifiwa barani Afrika lakini nayo ujio wake ulifuata mabadiliko ya Katiba. Tume za uchaguzi za Senegal na Malawi haziitwi huru kwenye majina yake lakini zimefanikisha kufanyika kwa uchaguzi ulio huru kwenye nchi zao ambapo wagombea wa upinzani walishinda pasipo mabadiliko ya Katiba.

Tanzania ni nchi tofauti na hizo mbili lakini inaweza kufuata njia zao. Ni nchi inayofanya uchaguzi na kupitisha sheria zake bungeni kama misingi ya kidemokrasia inavyotaka. Lakini bado inaitwa ya demokrasia-nusu kwa sababu inaonekana bado chama tawala kinapata upendeleo maalumu kwenye uchaguzi.

Nchini Senegal, siri ya tume yao ni kuwa na wajumbe wanaofahamika kwa maadili na wasiohusishwa na vyama vya siasa. Siri ya Malawi ni kuwa na mahakama na jeshi la nchi vyenye weledi na uzalendo kwa nchi na katiba yao.

Katika muktadha wa Afrika, suala la nani wanaongoza tume ya uchaguzi na taasisi za haki ni la muhimu kwa taswira ya uhuru wa tume kuliko jina lenyewe.

Kama serikali ya Rais Samia imedhamiria kuleta siasa za tofauti kwa kuanza na tume huru na inayoaminika, ni muhimu kwanza ikamaliza suala hili kwa kuwa na wajumbe wa tume wanaokubalika na wadau wa siasa na wanaoendana na matakwa ya sheria mpya.

Jina la tume ni muhimu, lakini wanaounda tume na utendaji wao katika misingi ya haki pasi na uependeleo ni muhimu zaidi.

Katika mazungumzo yangu na Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA), Tike Mwambipile, aliniambia changamoto kubwa iliyopo ni kuwa wajumbe na watumishi waliopo sasa wana mikataba halali kisheria na hawawezi kuondolewa tu kwa sababu ya kuundwa sheria mpya na kwamba ni lazima kuwepo na utaratibu wa namna ya kuwabadili.

Lakini Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Isihaka Mchinjita, anaamini kama serikali ina nia ya dhati ya kuhakikisha uchaguzi unasimamiwa na tume huru, inaweza kuweka utaratibu wa kuondoa wajumbe waliopo sasa na kupata wajumbe wapya haraka. Hili, kwa mujibu wa mwanasiasa huyo, ni suala la dhamira na nia njema kwa upande wa chama tawala.

Hata hivyo, dhamira na nia njema hiyo ya chama tawala inategemea kwa kiwango kikubwa tathmni ya ndani ya chama hicho kuhusu mustakabali wake katika uchaguzi ulio karibu wa serikali za mitaa 2024 na uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani wa mwaka 2025. Kwamba CCM itatekeleza dhamira yake hata kama inahatarisha kupungua kwa kura na viti vyake vya uwakilishi, achilia mbali kushindwa uchaguzi hilo ni suala la kulingojea kwa hamu kulishuhudia.