Benjamin Netanyahu amemwambia Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza David Cameron kwamba Israel "itafanya maamuzi yake" kuhusu jinsi ya kujibu mashambulizi ya Iran.

Alisema serikali yake "itafanya kila linalohitajika kujilinda" wakati wa mazungumzo ambayo serikali ya Uingereza ilitarajia itasaidia kuzuia kuongezeka kwa mzozo huo.

Bw Netanyahu ameapa mara kwa mara kulipiza kisasi shambulio hilo ambalo halijawahi kushuhudiwa kwa makombora na ndege zisizo na rubani mwishoni mwa juma.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Jerusalem baada ya mkutano na Bw Netanyahu, Bwana Cameron alisema yuko pale "kuonyesha mshikamano wetu" baada ya shambulio "baya" la Iran.

Aliendelea kusema: "Tunatumai kuwa kila kitu ambacho Israel hufanya kina kikomo na lengo na busara iwezekanavyo.

"Si kwa manufaa ya mtu yeyote kwamba tunaona ongezeko la hili na hilo ndilo tulilosema waziwazi kwa watu wote ambao nimekuwa nikizungumza nao hapa Israel."

Baada ya mkutano huo, waziri mkuu wa Israel alisema: "Nataka kuweka wazi - tutafanya maamuzi yetu wenyewe, na Taifa la Israel litafanya kila linalowezekana kujilinda.