Rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma yuko huru kugombea katika uchaguzi mkuu wa mwezi Mei baada ya mahakama ya uchaguzi kubatilisha marufuku ya kuwania urais.

Mwezi uliopita tume ya uchaguzi ilimzuia kwa kudharau hukumu ya mahakama.

Ilisema katiba inazuia watu kushikilia ofisi ya umma ikiwa watapatikana na hatia ya uhalifu na kuhukumiwa kifungo cha zaidi ya miezi 12 gerezani.

Bw.Zuma, 81, amekuwa akifanya kampeni kwa ajili ya chama kipya cha Umkhonto we Sizwe (MK). Kigogo wa zamani wa chama tawala cha African National Congress (ANC), alikua rais kuanzia mwaka 2009 hadi 2018, alipolazimika kung'atuka kwa tuhuma za ufisadi. Alihukumiwa kifungo cha miezi 15 jela mwaka wa 2021 kwa kukosa kutoa ushahidi katika uchunguzi wa ufisadi, ingawa alitumikia miezi mitatu tu kwa sababu za kiafya.

Hukumu hiyo inaweza kuwa na athari kubwa kwa matokeo ya uchaguzi wa mwezi ujao.

Bw Zuma ni kioo cha chama kipya cha upinzani cha MK, ambacho kimepewa jina la tawi la zamani la kijeshi la ANC. Rais huyo wa zamani anajiona kama mrithi wa kweli wa mizizi ya mapinduzi ya ANC, iliyowahi kuongozwa na Nelson Mandela.

Ushindi wa Bw Zuma katika mahakama unamaanisha kuwa sasa anaweza kugombea kama mgombea mkuu wa MK.