ANNE Makinda ni Spika wa Bunge Mstaafu, mwanasiasa maarufu, mwanamke aliyeitumikia serikali, chama cha TANU (Tanganyika African National Union) na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa takribani miaka 50 kuanzia ngazi ya chini kati ya miaka ya 1965 na 1975 na pia, amewahi kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa Mwaka 1977.

Amewahi kuteuliwa kuwa mkuu wa mkoa katika Serikali ya Awamu ya Kwanza chini ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Aliteuliwa kuwa mbunge katika Serikali Za Awamu ya Kwanza na Awamu ya Pili chini ya Ali Hassan Mwinyi kati ya mwaka 1975 na 1995.

Baadaye kati ya mwaka 1995 na 2015, alikuwa mbunge wa kuchaguliwa katika Jimbo la Njombe Kusini.

Wakati anaendelea na ubunge, aliteuliwa na Rais wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma. Hii ni kati ya mwaka 1995 hadi 2000.

Hayati Edward Sokoine

Katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2000, alishinda Ubunge wa Njombe Kusini kwa mara ya pili na ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akapewa jukumu la kuongoza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maliasili, Mazingira na Kupambana na Umasikini.

Aidha, Anne Makinda amewahi kuwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto.

Ni Naibu Spika wa kwanza mwanamke katika Bunge la Tanzania katika kipindi cha kati ya mwaka 2005 na 2010 na pia ni Spika wa Kwanza mwanamke wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanzia mwaka 2010- 2015.

Anasema aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Februari, 1983 na hiyo, ilikuwa kwa mara ya kwanza kufanya kazi Sokoine na walidumu kwa mwaka mmoja hadi Aprili 12, 1984 Edward Sokoine alipofariki dunia kwa ajali ya gari.

Mwanasiasa huyu maarufu licha ya kushika nyadhifa hizo za kiserikali, Kimataifa aliwahi kuwa Mwenyekiti wa na Rais wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF), kati ya mwaka 1993 na 1994.
Amewahi kuwa mwenyekiti na mjumbe wa bodi mbalimbali nchini. Mwaka 2022 aliteuliwa kuwa Kamishina wa Sensa ya Watu na Makazi.

Huyo ndiye Anne Makinda. Anaeleza haya kwenye mdahalo wa kitaifa wa Kumbukizi ya Miaka 40 ya Hayati Sokoine uliofanyika Aprili 8, 2024 katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) mkoani Morogoro ukibeba kaulimbiu isemayo: ‘Urithi wa Taifa katika Uongozi Wake, Bidii, Udilifu na Uaminifu.’

Mdahalo huo wa kitaifa ulifunguliwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko akimwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi.

Anasema akiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, alifanya kazi kwa karibu na Edward Moringe Sokoine aliyekuwa Waziri Mkuu kabla ya kifo chake.

Spika wa Bunge mstaafu, Anne Makinda

Anaeleza namna alivyofanya kazi na Hayati Sokoine yeye (Makinda) akiwa Waziri Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu na kuwa ni miongoni mwa mawaziri wake wa mwisho hadi siku ya kifo chake.

Anasema alifanya naye kazi Sokione alipoteuliwa kuwa Waziri Mkuu kwa mara ya pili na katika nyakati hizo, taifa lilikuwa ndio kwanza limetoka katika Vita ya Kagera iliyomg’oa Iddi Amin nchini Uganda alipovamia ardhi ya Tanzania.

Kwa mujibu wa Makinda, katika kipindi hicho Tanzania pia ilikuwa haikubaliani na masharti ya Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), hali iliyosababisha kuwepo kwa uhaba wa bidhaa muhimu na kutokea kwa biashara za ulanguzi na wahujumu uchumi.

Anasema: “Katika kipindi chake cha pili wakati ameteuliwa (Sokoine) kuwa waziri mkuu, hali ya nchi haikuwa nzuri na hakukuwa na bidhaa muhimu… “

Akiwa Waziri wa Nchi ,Ofisi ya Waziri Mkuu kuratibu mambo yote ya kiserikali, serikali iliamua kuanzisha kampuni za biashara za mikoa zilizojulikana kama RTC kusimamia ugawaji wa bidhaa zinazozalishwa katika viwanda vya ndani.

Anasema licha ya kuanzishwa kwa RTC kusimamia ugawaji wa bidhaa zilizokuwa zinazalishwa na viwanda vya ndani, baadhi ya viongozi walitumia nafasi zao kujinufaisha kwa kuchukua bidhaa muhimu kutoka RTC na kuwauzia baadhi ya wafanyabiashara wenye uwezo wa kifedha.

“Hiyo,” anasema ndio iliyosababisha kuwapo biashara kubwa ya ulanguzi nchini.

“Siku moja katika mahangaiko haya nafikiri siku ya Pasaka nikiwa kanisani, kikaja king’ora cha polisi pale kanisani nikatoka kanisani na kungia kwenye gari la polisi hadi ofisini kwa waziri mkuu. Nikakuta kikao kizima cha kamati ya ulinzi na usalama wamekuwa ‘full’ kikazi,” anasema Makinda.

Anafafanua kuwa, baada ya kufika ofisini, Waziri Mkuu (Sokoine) akamwambia (yeye Makinda) kuwa atakuwa Mwenyekiti wa Mali za Walanguzi nchi Nzima.

“Nilikuwa sijui mali za walanguzi ni cheo gani, kimetoka wapi! Kuuliza nikashindwa na ilipofika asubuhi yake, ikabidi nimuulize katibu wangu hiki kitu mali za walanguzi ni kitu gani,” anasema Makinda na kuongeza kuwa, hapo ndipo ilipoanzia vita ya kupambana na walanguzi na wahujumu uchumi nchini.

Anasema kikubwa ambacho hayati Sokoine alikuwa akikisimamia wakati wote kwa mtumishi wa umma, ni utayari wakati wote.

“Kwa upande wangu nikiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu licha ya kupagiwa majukumu mengine, nilikuwa ninampatia taarifa ya hali ya nchi kila siku na ikiwa na ufuatiliaji wa matukio,“ anasema Makinda.

Spika mstaafu huyo anasema hata asubuhi ya siku ile aliyofariki Sokoine, mawaziri wa ofisi yake na watumishi wengine wote walifika kazini (ofisini) na Sokoine aliwapa taarifa kuwa amepiga simu nchi nzima. Katika nyakati hizo kulikuwa na ukame mkubwa. Sokoine akawaambia asubuhi hiyo kuwa siku hiyo mvua ilikuwa imenyesha kila mkoa.

Anasema baada ya kuwaambia hali ya mvua kunyesha katika mikoa yote, alisimama mlangoni na akawaaga mmoja mmoja wafanyakazi wa Ofisi ya Waziri Mkuu.

“Kwangu mimi akaniambia subiri. Akaniambia kuwa mafaili ya wahujumu uchumi yote nimeyamaliza ndipo na tukaagana pale, lakini baada ya saa moja akapata ajali na kufariki dunia,“ anasema Makinda.

Makinda anasema wanachojifunza kutoka kwa Sokoine ni nidhamu ya kazi, kujali muda, wote ni kazi na ukiwa kiongozi unapopingiwa simu uwe unapatikana na jambo lingine ni la uadilifu.

“Katika suala la uadilifu siku moja sikumbuki vyema mheshimiwa mmoja alileta zawadi kwa waziri mkuu akidhani yenye ni mfugaji. Alileta ng’ombe aliyekuwa amefungwa kamba. Sokoine akamuuliza huyu ng’ombe umemleta kwa Sh ngapi na yule mheshimiwa akasema hapana mheshimiwa hii ni zawadi yako mzee. Cha ajabu, Sokoine akaandika kiwango cha fedha kwenye hundi akampa yule bwana,“ anasema Makinda.

Kwa mujibu wa Makinda, hayati Sokoine alikuwa hapokei zawadi na pia, alikuwa na desturi kukataa masuala kuletewa umbea.

“Ukimfikishia umbea, yeye alikuwa ana nyamaza tu,” anasema Makinda na kuongeza: “lakini siku inayofuatia, anamwita mtu yule uliyemfikishia umbea na mtoa umbea na kuwakutanisha ofisini kwake ili yaliyosemwa yaelezwe bayana wote wakiwepo… “

Spika mstaafu Makinda anamtaja Sokoine kama kiongozi aliyekuwa mcha Mungu, aliyesali na hasa katika vipindi vya sikukuu za Pasaka na Krisimasi. Anasema: “Hata siku aliyokufa Sokoine, alitoka kusali kanisani.”

Anasema wakati akiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, alikuwa anasimamia Bunge na siku moja ndani ya bunge baadhi ya mawaziri walishindwa majibu ya maswali ya wabunge.

“Yalikuwa kama maswali sita na mawaziri hawakuwa na majibu. Ndipo Waziri Mkuu Sokoine aliposimama kuwatahadharisha kuwa atamfukuza kazi waziri yeyote atakayeshindwa kutoa majibu ya maswali bungeni,” anasema Makinda.