DODOMA: SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) limefafanua kuwa Mradi wa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere (JNHPP) limechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza athari za mafuriko katika maeneo ya Wilaya za Rufiji na Kibiti, tofauti na kinyume chake inavyoripotiwa kuwa mradi huo umechangia kutokea kwa mafuriko hayo.

Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano na Uhusiano kwa TANESCO, Makao Makuu Dodoma leo imeeleza kuwa kitakwimu inaonesha kuwa maeneo ya Rufiji na Kibiti mkoani Pwani yamekuwa yakikumbwa na mafuriko kwa miaka mingi ya nyuma kwa kiwango kikubwa kuliko hali ilivyo hivi sasa.

“Kama mradi wa JNHPP usingejengwa basi maji haya yangefika moja kwa moja kwenye maeneo ya Rufiji na Kibiti na hivyo kusababisha athari kubwa zaidi,” imeeleza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa athari za mafuriko zinazoonekana sasa zimechangiwa kwa kiasi kikubwa na mvua za El-nino zinazoendelea kunyesha tangu mwaka jana hivyo kupelekea mafuriko katika maeneo mbalimbali nchini.

“TANESCO inakanusha taarifa zozote za upotoshaji zinazohusisha bwawa la Julisu Nyerere na mafuriko ya Kibiti na Rufiji na linakemea upotoshaji unaofanywa na baadhi ya watu wasio na nia njema kubeza juhuhudi za serikali katika kuimarisha hali ya upatikanaji wa umeme nchini kwa ujenzi wa bwawa la Julius Nyerere,” imekemea taarifa hiyo.