Mamlaka ya Ujerumani inasema kuwa imewakamata watu watatu kwa tuhuma za ujasusi wa China.

Mshukiwa mkuu aliyetajwa kwa jina la Thomas R, anatuhumiwa kufanya ujasusi wa Wizara ya Usalama ya Nchi ya China.

Waendesha mashtaka wanadai mtandao wake uliendesha kampuni ambayo ilishirikiana na mashirika ya utafiti ya Ujerumani.

Washtakiwa hao wanadaiwa kukusanya taarifa nyeti, ikiwamo miundo ya injini inayofaa kutumika kwenye meli za kivita ili kupeleka China.

Katika hatua tofauti, wanaume wawili nchini Uingereza walishtakiwa kwa ujasusi wa China baada ya kushutumiwa kutoa taarifa ambazo zinaweza "kuwa na manufaa kwa adui", kulingana na polisi.

Katika kesi ya Ujerumani, waendesha mashtaka wanadai Thomas R alipata "teknolojia ya kibunifu kwa matumizi ya kijeshi" kwa niaba ya mfanyakazi wa Wizara ya Usalama ya Nchi ya China.

Pia wanadai alitumia kampuni - inayoendeshwa na washukiwa wengine wawili, walioitwa kama Herwig F na Ina F - ambayo iliwasiliana na watu wanaofanya kazi katika sayansi na utafiti.

Mradi wa kwanza kuhusu uendeshaji wa injini za baharini zenye ufanisi mkubwa kwa matumizi ya meli za kivita unadaiwa kuwa tayari umekamilika.