ALIYEKUWA Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambaye kwa sasa amejiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mchungaji Peter Msigwa amewataka Watanzania kuachana na vyama vya upinzani ambavyo kazi yao ni kupiga porojo na kupinga maendeleo.

Aidha amewataka Watanzania kumuunga mkono Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwani ni kiongozi ambaye tangu ameingia madarakani ameonesha dhamira ya dhati ya kuwatumikia Watanzania na kuleta maendeleo sambamba na ujenzi wa uchumi imara wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Mchungaji Msigwa ameyasema hayo leo Agosti 27,2024 alipokuwa akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Kigamboni mkoani Dar es Salaam katika mkutano wa hadhara wakati wa ziara ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM CPA Amoss Makala ambaye anafanya ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani na kusikiliza kero za wananchi wa Mkoa huo.

Akizungumza mbele ya wananchi Mchungaji Msigwa aliyekuwa Mbunge wa Iringa Mjini kwa miaka 10 kupitia CHADEMA amesema kwamba takribani miaka 20 iliyopita alikuwa CHADEMA na kwamba Chama hicho kiliaminisha wananchi kinapambana na demokrasia na kupinga ufisadi.

"Lakini baada ya muda mrefu aligundua Chama cha CHADEMA ni SACCOS ya mtu.Kupitia CHADEMA hicho tumekuwa tukiwahamasisha vijana kuandamana na wengine walikufa, watu wameingia kwenye migogoro.

"Kumbe Chama kilikuwa mali ya mtu, tukiwa Bungeni tulikuwa na kiongozi wa Kambi ya Upinzani  Bungeni(Freeman Mbowe) lakini hakuna alichokifanyaAmekuwa  akikimbia vyombo vya habari,kila akiitwa haendi lakini vikitokea vyombo vya habari vya nje ndio anakwenda ili kusema vibaya nchi."

"Achaneni na vyama vya upinzani ambavyo kazi yake ni kupiga porojo. Sote tunaona namna ambavyo Rais Dk.Samia ambavyo amedhamiria kuleta maendeleo.Rais Samia yuko siarasi na ndio maana anapambana kujenga uchumi wa nchi pamoja na uchumi wa Jiji la Dar es Salaam.Mama Samia anaonesha muelekeo mzuri wa kujenga Taifa letu, tumuunge mkono."

Aidha amesema yeye kwa sasa mashambulizi yake  yanakwenda upinzani kwani  nimerudi Chama Cha Mapinduzi, kuhamasisha akina mama achaneni na porojo za upinzani.Tulipinga SGR, Bwawa la Mwalimu Nyerere na miradi mingine ya maendeleo.

"Tulipinga kila kitu, leo SGR imekamilika unasafiri kutoka Dar es Salaam adi Dodoma unatumia saa nne badala ya saa nane kwa basi."Tumuunge mkono mama Samia, tuiunge mkono CCM ili kuleta maendeleo,"amesema na kuongezea tangu Rais Samia aingie madarakani uchumi umekuwa kutoka asilimia nne mpaka asilimia 5.2."