SERIKALI imeanza kugawa eneo jipya kwa ajili ya makazi ya wananchi waliokumbwa na mvua za El-Nino katika kata ya Mohoro Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani.

Hayo yamebanika wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira katika maeneo yaliyoathiriwa na mvua za El-Nino ya kata ya Mohoro katika Wilaya ya Rufiji mkoani humo.

SOMA: ‘Mafuriko Rufiji chanzo si Bwawa la Nyerere’ …

Akizungumza na wananchi hao, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Khamis Hamza Khamis ametoa wito kwa wananchi kutofanya shughuli zinazochangia uharibifu wa mazingira ya bahari na badala yake waitunze.

Pamoja na kutoa pole kwa waathirika wa mafuriko, naibu waziri huyo amewaomba wananchi kuacha kuvua kwa kutumia uvuvi usio rasmi ambao unachangia kuua viumbe vya baharini na makazi ya samaki.

Aidha amewataka wananchi kuacha kuvamia maeneo yaliyohifadhiwa kwa kuchoma misitu na kukata miti kwa ajili ya kuni na mkaa kwani vitendo hivyo vinaharibu mazingira na hivyo kusababisha mabadiliko ya tabianchi ambayo huleta mafuriko.