ITALIA : WAFANYAKAZI wa uokoaji wamepata miili 5 Jumatano ndani ya boti ya kifahari ya Bayesian, ambayo ilizama Jumatatu kwenye pwani ya Sicily, Kusini mwa Italia.

Boti hiyo ya kifahari yenye urefu wa mita 56 iliyokuwa ikipeperusha bendera ya Uingereza ilikuwa imebeba watu 22, akiwemo bilionea wa Uingereza na mtendaji mkuu wa benki ya Morgan Stanley.

Bayesian ilizama katika dhoruba kali mapema Jumatatu asubuhi ambapo watu 15 waliokuwa ndani yake waliokolewa huku mtu mmoja alipoteza maisha..

SOMA: Watu kadhaa wahofiwa kufa ajali ya boti Cape Verde

Watu ambao bado hawajapatikana wametajwa kuwa ni tajiri wa teknolojia wa Uingereza Mike Lynch na binti yake mwenye umri wa miaka 18 Hannah; Mwenyekiti wa Kimataifa wa kampuni ya Morgan Stanley Jonathan Bloomer na mkewe Judy Bloomer; Chris Morvillo, Wakili wa Marekani wa Lynch, na mkewe Neda Morvillo.