Asilimia 30 mpaka 40 ya wanawake wanaohudhuria kliniki hospitalini hapo wana tatizo hilo
  • Author,

"Kwa kweli tumefurahi sana kupata huduma ya aina hii hapa nchini, na hasa katika hospital yetu ya taifa Muhimbili, kwa sababu watu wetu wengi uwezo wa kusafiri nje hawana, hivyo tunapopata huduma hii karibu, tunahisi hata gharama kidogo zitapungua, ukilinganisha na zile ambazo wangetumia kwenda kupata matibabu nje ya nchi. Ni huduma ya muhimu na hili tatizo la uzazi lipo, wengi linawakabili’’

Ni kauli ya mkaazi wa jiji la Dar es Salaam, eneo la Kivule Boniface Renatus Mwapili, ambaye nilikutana naye akitafuta huduma na maelekezo, katika kituo cha upandikizaji mimba katika hospital ya taifa Muhimbili, huku akiweka matumaini yake kwa kituo hicho kuwasaidia wenye changamoto za kupata watoto na wana uhitaji wa huduma hiyo.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi mtendaji wa Hospital ya Taifa Muhimbili, Profesa Mohammed Janabi, familia kushindwa kupata mtoto asilimia 35 ni tatizo linatokana kwa upande wa wanaume na asilimia 65 ni kwa upande wa wanawake.

Professa Janabi anatolea mfano kuwa asilimia 30 mpaka 40 ya wanawake wanaohudhuria kliniki hospitalini hapo wana tatizo hilo ambalo linasababisha migogoro na misononeko kwenye familia.

Hali hiyo ndiyo inamtisha pia mkazi huyo wa Kivule, Boniface Renatus Mwapili, ambaye anakiri pia tatizo la uzazi kuwa ni kubwa.

‘’kwa sababu sisi tunachojua mtu akishaolewa baada ya mwezi ama miezi miwili tayari ameonesha dalili ya ujauzito, sasa anapochukua muda mwingi bila ya kushika mimba, jamii nyingi za kiafrika ni ngumu kuvumilia, utaanza kupata matatizo hasa kutoka kwa mawifi au kwa wakwe, kwamba sasa wewe umekuja tu kutia hasara, na migogoro huanzia hapo.

KWANINI KITUO HICHO SASA?
H

CHANZO CHA PICHA,MUHIMBILI HOSPITAL

Maelezo ya picha,Kwa sasa wagonjwa 10, wako tayari kuanza huduma hii

Dkt. Geofrey Simon Marandu ni mkuu wa idara ya wanawake na uzazi katika hospitali ya taifa Muhimbili anasema kutokana na changamoto hiyo wameona ipo haja ya kuwa na kitengo kama hicho kwa hospital za umma, na kwamba Muhimbili imekuwa ya kwanza kwa hospital za umma nchini Tanzania.

Anasema matatizo ya uzazi yamekuwepo kwa muda mrefu na yalikuwa yakitatuliwa kwa namna tofauti, kama vile upasuaji, upasuaji wa mirija, lakini kwa wenye uwezo na ambao walikuwa wakihitaji huduma hiyo, waliifuata nje ya nchi kwa gharama kubwa.

Na baadaye hospital chache binafsi nchini Tanzania zilianzisha huduma hizo, lakini gharama bado ziko juu kwa wananchi wa kawaida.

‘’Hatimaye ufumbuzi umepatikana kwa hospitali ya taifa kuanza kutoa huduma hii, angalau bei itapungua kwa kiasi kikubwa, na itapungua zaidi pale ambapo serikali itakapotoa vibali vya kuingiza kama vile dawa na baadhi kuondolewa kodi, ili dawa zinazotumika ziwe na bei ya chini, ameeleeza Dkt. Marandu.

‘’Mpaka sasa watu wengi wameshaulizia huduma hiyo katika hospitali ya taifa Muhimbili na kliniki zimeshaanza kwenye vitengo, wana wagonjwa wengi tu… na wameshafika zaidi ya wagonjwa 78, lakini kwa sasa wagonjwa 10, wako tayari kuanza huduma hii, kwa sababu hawawafanyiwi wote kwa pamoja, wanakwenda kwa awamu’’.

Kwa mujibu wa daktari huyo bingwa, walengwa wa huduma hiyo ni wanawake na wanaume, ambao hawana uwezo wa kutungisha mimba kwa njia ya kawaida na hata ya upasuaji.

Hata hivyo, anasema si tu wanaoshindwa kutungisha mimba tu, lakini hata wale ambao wanapata tatizo ya kiafya na wanataka mbegu zao kuvunwa na kuhifadhiwa kwa ajili ya kuweza kutumika tena baadaye.

”Kwa hiyo ni huduma pana zaidi kuliko tunavyoichukulia, kwenye nchi za wenzetu unaweza kuta kuna mtu amepata matatizo na kuhukumiwa kifungo cha muda mrefu, na hajui atatoka lini.., anaweza kutoa mbegu zake akazihifadhi, na pindi anapotoka na kutaka kuzaa basi zinatumika mbegu zake hizo, alizohifadhi wakati akiwa na umri mdogo’’, anasema Dkt. Marandu.

Dondoo zaidi za kitaalamu na gharama kwa wahitaji

H

CHANZO CHA PICHA,MUHIMBILI HOSPITAL

Maelezo ya picha,Gharama za matibabu katika huduma hiyo ya upandikizaji katika hospitali ya taifa Muhimbili ni shilingi milioni 13 za Tanzania

Dokta Matilda Michael Ngarina, ambaye ni bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi na mbobevu katika kumsaidia mtu kupata ujauzito amenieleza pia kwa nini wameamua kuanzisha huduma hiyo, katika hospitali ya umma Muhimbili.

‘’Inafika mahali unakuwa na mgonjwa unatibu lakini unaona unafika mwisho, mirija imeziba unamsaidiaje labda amepata hatari ya mimba nje ya mirija ya uzazi mara mbili (Ectopic Pregnancy) na ana hamu ya kupata mtoto, na hana uwezo wa kwenda nje ama hospitali binafsi.

Ameongeza: Kwa hiyo tukasema labda na sisi tukianzisha tukajaribu kujibana tunaweza kusaidia watu wenye uhitaji na wenye uwezo mdogo kwenda nje ama hospitali binafsi.

Gharama za matibabu katika huduma hiyo ya upandikizaji katika hospitali ya taifa Muhimbili ni shilingi milioni 13 za Tanzania ambazo ni takribani sawa na dola Marekani 4,810.

‘’Tulipiga hesabu za kila kitu lakini mwishowe, tulikuja kufika milioni 13, kwa sababu chini ya hapo ina maana sasa labda serikali ifidie tuweze kupata dawa, ama serikali ifidie vitu vingine ambavyo vinahitajika kuweza kupata huduma’’, alimefafanua Dkt. Ngarina.

Nilipomdadisi zaidi, Dkt. Ngarina kwa wanawake na wanaume kushindwa kutungisha ama kutunga mimba liko kwa kwa kiasi gani, aliniweka wazi.

”Labda niseme kwamba moja ya tatu ya matatizo yanatoka kwa mwanaume na moja ya tatu kwa mwanamke lakini kuna moja ya tatu ambayo hatujui, maana utamkuta mama hana shida na baba hana shida lakini hawapati mimba, kwa hiyo suala la uzazi nadhani pia lina u-Mungu ndani yake, lakini pia kuna vitu unaweza kuvikuta kwa mtu ukajua hili ni tatizo na hili si tatizo.’’

Wahitaji wa huduma hii ni akina nani hasa?

H

CHANZO CHA PICHA,MUHIMBILI HOSPITAL

Maelezo ya picha,Lakini pia kuna masharti mengine kwa mwanamke kabla ya kupata huduma hizo.

Dkt. Matilda Ngarina anasisitiza kuwa si kila mwanamke ambaye hapati mtoto anatakiwa apandikizwe, akifafanua kuwa kati ya wanawake wanne ambao hawapati mtoto inaweza kuwa ni mmoja tu ndiye anahitaji kupandikizwa, huku wengine wakiweza kutibiwa tu katika kliniki ya kawaida.

Kuna maandalizi kadhaa kabla ya mwanamke hajapandikizwa mbegu kwani mchakato mzima unaweza kuchukua takriban miezi miwili.

Dkt. Ngarina anasema kila hatua kabla ya kufanyiwa upasuaji inakuwa na maelekezo yake.

Lakini pia kuna masharti mengine kwa mwanamke kabla ya kupata huduma hizo.

‘’Kipindi hicho hutakiwi kukutana na mwanaume unatakiwa kuwa msafi na ikifika kipindi cha kupandikizwa pia kabla hujaingia chumba cha upasuaji kuna maelekezo yake pia unatakiwa ufanye nini, usile vyakula vibaya usichoke, usilewe, ili mwili uwe safi kwa ajili ya kupokea kiumbe, pamoja na utulivu.

Mtaalamu huyo pia amefahamisha kuwa mbegu zinaweza kuhifadhiwa kwa muda mrefu, lakini muda unavyozidi kwenda zinaweza kupoteza ubora.

Wakati akizindua huduma hiyo, Makamu wa Rais wa Tanzania Dokta Phillip Mpango alisema uwepo wa kituo hicho cha upandikizaji mimba ambacho ni cha kwanza kwa hospitali za umma nchini Tanzania kutawasaidia kwa kiasi kikubwa wananchi ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakipata changamoto mbalimba za kupata watoto.

Lakini swali muhimu la kujiuliza ni kwamba, bila msaada wa serikali ni watu wangapi wa kipato cha chini wenye kuhitaji huduma hiyo, wataweza kupata matibabu hayo kutokana na gharama yake ya shilingi milioni 13, licha ya kuwa ndiyo gharama ya chini ikilinganishwa na ile inayotozwa katika hospital binafsi na nje ya nchi?.