Chidimma Adetshina sasa ataiwakilisha Nigeria katika shindano la Miss Universe la Novemba

Baada ya kuandamwa juu ya uraia wake na kulazimishwa kujiondoa kwenye shindano la Afrika Kusini, Chidimma Adetshina ametawazwa kuwa malkia wa urembo wa nchi tofauti kabisa.

Bi Adetshina alilia machozi ya furaha alipotangazwa kuwa Miss Universe Nigeria siku ya Jumamosi.

"Taji hili si la urembo tu; ni wito wa umoja," mwanafunzi huyo wa sheria mwenye umri wa miaka 23 alisema hayo baada ya wiki ya kusakamwa na vyombo vya habari.

Alialikwa kushiriki Miss Universe Nigeria baada ya nafasi yake kama mshindi wa fainali katika shindano la Miss Afrika Kusini kuzua wimbi la ukosoaji.

Baadhi ya watu nchini Afrika Kusini walikuwa wametilia shaka kustahili kwake kushiriki mashindano hayo kwa sababu licha ya kuwa ni raia wa Afrika Kusini, baba yake Bi Adetshina ana asili ya Nigeria huku mama yake akiwa na asili ya Msumbiji.

Mzozo kuhusu uraia wake ulisababisha uchunguzi kufanyika huku waandaji wa Miss Afrika Kusini wakiitaka idara ya mambo ya ndani ya taifa hilo kuangalia kustahili kwake.

Baada ya uchunguzi wa awali, idara ilitangaza kuwa mama yake Bibi Adetshina huenda alifanya "wizi wa utambulisho" ili aweze kuwa raia wa Afrika Kusini.

Hata hivyo, taarifa hiyo iliongeza kuwa Bi Adetshina "hangeweza kushiriki katika madai ya vitendo vya kinyume cha sheria vya mama yake kwani alikuwa mtoto mchanga wakati huo".

Baada ya kusikia yaliomkuta Bi Adetshina, waandaaji wa Miss Universe Nigeria walimwalika kushiriki katika shindano lao.

Walisema ataweza "kuwakilisha nchi asili ya baba yake kwenye jukwaa la kimataifa".

Baada ya kushinda shindano hilo siku ya Jumamosi, Bi Adetshina atawakilisha Nigeria katika shindano la Miss Universe linalotarajiwa kufanyika mwezi Novemba mwaka 2024.

Mafanikio yake yamesherehekewa kwenye mitandao ya kijamii mbalimbali.