MKOA wa Tabora unatarajiwa kupata watumishi wapya zaidi ya 4,000 huku kada ya afya ikipata kipaumbele kikubwa kwenye mgawanyo wa watumishi hao.

Hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za serikali kupunguza upungufu wa watumishi katika sekta za umma, hasa katika Halmashauri ya Nzega na maeneo mengine yenye uhaba wa rasilimali watu.

Akizungumza wakati wa ziara yake Mjini Nzega, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deus Clement Sangu alibainisha kuwa ajira hizo ni sehemu ya kibali cha jumla cha kuajiri watumishi wapya 47,000 nchini Kilichotolewa na Rais Samia.

“Ajira hizo zitasaidia kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi katika sekta muhimu kama vile afya, elimu, na miundombinu. Tayari mchakato wa kuwapata watumishi wapya unaendela kwa kufuata utaratibu wa ajira kupitia Sekretarieti ya Ajira Katika Utumishi wa Umma,” amesema.

Naibu Waziri pia alitoa wito kwa watumishi wa umma kuwa wabunifu, wenye nidhamu na kufanya kazi kwa bidii ili kuendana na kasi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali. Alisisitiza umuhimu wa waajiri kuwa karibu na watumishi wao ili kuhakikisha migogoro isiyo ya lazima inazuiwa. “Watumishi mnatakiwa kutathmini utendaji wenu na kuboresha huduma mnazozitoa kwa wananchi,” amesema.