WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Stergomena Tax amewataka wakazi wa kijiji cha Chitoholi kilichopo kata ya Mkundi katika Halmashauri ya Wilaya Tandahimba mkoani Mtwara kutunza miundombinu ya maji.

Dk Stergomena amesema hayo leo Oktoba 7, 2024 katika uzinduzi wa mradi wa maji wa Chitoholi ambao utahudumia vijiji sita vilivyopo kwenye kata ya Mkundi na Chikongola katika halmashauri hiyo.

Stergomena amesema mradi huo una miundombinu ambayo inawezesha kusambaza maji kwenye vijiji sita hivyo amemtaka kila mwananchi kuhakikisha analinda miundombinu hiyo ili iendelee kutoa huduma na serikali iweze kutatua changamoto nyingine.

Akisoma taarifa ya mradi huo, Meneja wa Wakala wa Usambazaji wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wilayani Tandahimba Mhandisi Antidius Muchunguzi amesema mradi huo umetekelezwa ili kutatua adha ya upatikanaji wa maji safi na salama ambapo hapo awali walikuwa wanatembea umbali wa kilomita 5 hadi 8 kufuata maji.

SOMA: Kiongozi Mbio za Mwenge awafagilia RUWASA Mtwara

Kupitia mradi huo watu wapatao 10,817 watafikiwa na maradi katika kata hizo mbili ya Mkundi na Chikongola. Mradi huo umegharimu kiasi cha Sh bilioni 1 kwa ajili ya ujengaji wa tanki lenye ujazo wa lita 225,000 juu ya ardhi.

Pia ujenzi wa vioski 15, ujenzi nyumba ya pampu pamoja na kuunganisha huduma ya maji katika taasisi saba ambazo ni zahanati na shule pamoja na mengine.

Miongoni mwa wakazi wa vijiji hivyo ambao ni wanufaika wa mradi huo wameishukuru serikali kwa kuhakikisha inatatua kero ya wananchi kutembea umbali mrefu kwa ajili ya kufata maji.

Fadhiri Kaumbata mkazi wa kijiji cha Chitoholi ‘A’ wilayani humo amesema wameupokea mradi kwa mikono miwili na kuahidi kulinda miundombinu ya mradi huo.

“Tumeupokea vizuri mradi huu kwani hapo mwanzo ilitulazimu kuamka saa 9 au saa 10 kwa ajili ya kufata maji hivyo tutahakikisha tunautunza na kuulinda ili tuzidi kunufaika nao”