WAJASIRIAMALI wameonywa kutumia mikopo ya kausha damu na badala yake wametakiwa kutumia vizuri mikopo ya asilimia 10 ya halmashauri kukuza biashara zao.

Pia wametakiwa kujua matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii ili kutangaza biashara zao kisasa.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo ametoa wito huo mara baada ya kufunga mafunzo ya siku tatu kwa wajasiriamali 600 yaliyodhaminiwa na kufundishwa na wakufunzi katika Chuo cha Biashara (CBE) Wilaya ya Ilala Dar es salaam.

“Mikopo ya kausha damu imekua na athari kwa jamii kutokana na masharti ya urejeshaji na imekuwa ikisababisha migogoro katika familia nyingi hali inayosababisha umaskini zaidi,” amesema Mpogolo.

Mpogolo amesema Wilaya ya Ilala ina zaidi ya Sh bilioni 11 kwa ajili ya kuwezesha na kutoa fursa hiyo kwa makundi ya wanawake, vijana na walemavu ili waweze kujiendeleza kiuchumi.

Ameongeza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan amerudisha fursa hiyo kwa makundi hayo ili yaweze kukuza biashara zao.

SOMA: DC Ilala atoa elimu uchaguzi mitaa

Ameeleza kuwa kupitia mikopo hiyo kundi kubwa la wanawake watanufaika kwa kuwa wana muamko wa vikundi tofauti na kundi la wanaume ambao ni wachache waliojikita katika vikundi vya uwekaji fedha.

Amesema kwa sasa mikopo hiyo itatolewa kwa makundi matatu katika viwango tofauti kwa waombaji kuanzia kiasi cha Sh 500,000 hadi Sh milioni 10 kwa kundi la kwanza, kundi la pili Sh milioni 10 hadi milioni 50 na kundi la tatu milioni 50 hadi 150.

Sambamba na hayo amesema kupitia mafunzo waliyopata kwa siku tatu juu ya elimu ya masoko waweze kutafuta masoko mapya hasa kwa wafanyakazi maofisi ili kuwafikishia mahitaji kwa urahisi.

Mpogolo amewataka wanufaika wa mafunzo hayo kuyatumia vizuri ili kuleta tija katika biashara zao kwa kuwa wabunifu zaidi ili kuongeza ufanisi katika biashara zao na kuacha kutumia mikopo hiyo katika mambo ya anasa.

Amewahimiza kutumia njia rafiki ya kufunga bidhaa zao kulingana na uhitaji wa mteja na bei ya soko ili wateja waweze kumudu kununua tofauti ya soko la sasa kuangalia mteja mmoja.

Amesema asilimia 90 ya wafanyabiashara wa Halmashauri ya Jiji la Ilala inawateja wanaotoka katika nchi jirani, mikoani na wilaya nyingine ndani ya Dar es salaam hali ambayo inalrta ushindani katika masoko kufanya wawe na uhitaji wa mikopo ya uhakika.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Biashara CBE, Prof Edda Lwoga amesema wameamua kudhamini na kufundisha mafunzo hayo ya siku tatu ili kuongeza uelewa kwa wajasiriamali kufanya biashara zao kisasa na kukuza uchumi.