KATIBU wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, CPA Amos Makalla amewataka watu kuondokana na dhana kuwa chama tawala kikishinda kuwa sio demokrasia kwani CCM pia inachaguliwa na watu kutokana na kazi zake inazozifanya.
CPA Makalla ameeleza hayo leo Novemba 29, 2024 katika mkutano alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi ndogo ya CCM Lumbumba Dar es salaam.
Makalla amesema uhalali wa ushindi wao unategemea wananchi kutokana na kazi nzuri wanazofanya hususani katika utekelezaji wa ilani ya uchaguzi na utatuzi wa kero za wananchi.
Ameongeza CCM Inakemea na kulaani matukio yaliyojitokeza katika uchaguzi huo na kusisitiza matukio hayo yasihusishwe na vyama vya upinzani tu kwani yanatokea kwa wote, hivyo wanakemea mauaji nchi nzima.
“CCM inamakada sita waliofanyiwa vitendo vya kupiga, kujeruhiwa na kuuwawa na nyie ni mashahidi tarehe 13 mwezi wa 11 mwaka huu katibu wa CCM Wilaya ya Kilolo Iringa, Christina Kibiki iuwawa kwa kupigwa na risasi nyumbani kwake,” amesema Makalla.
Ameongeza kuwa makada wengine wanne Rolia na Tarime, wamejeruhiwa vibaya na mwingine mkoani Songwe alipigwa na ncha kali katika kipindi cha uchaguzi na bado yupo hospitali mahututi.
Pia amesema anatambua kuwa uchaguzi huo ulikuwa na changamoto mbalimbali zilizojitokeza na kuwasisitiza viongozi wa vyama vyote vya siasa kushirikiana ili waweze kutatua changamoto hizi zisijirudie katika chaguzi zijazo.
“Tunatambua kwamba zipo changamoto mbalimbali zilizojitokeza katika uchaguzi huu lakini tushirikiane vyama vya siasa ambao ni wadau kuhakikisha na sisi tunakuwa sehemu ya kutatua changamoto hizo hususani katika wakati wa uteuzi wa wagombea,” amesema Makalla.
Amesisitiza kuwa uchaguzi unaokuja wafanye kazi ya elimu kuhakikisha wahakikishe mambo yanakwenda sawa hususani katika wakati wa kujaza fomu na kuwataka waendelee kujenga vyama vyao kwa kutoa mafunzo na kutatua migogoro bila kuchoka.
0 Comments