Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu amekabidhiwa leo ofisi yake na Katibu Mkuu wa chama hicho John Mnyika, mikocheni jijini Dar es Salaam.
Wakati wa kukabidhiwa ofisi hiyo, Lissu alikuwa na makamu wake John Heche na Naibu Katibu Mkuu Bara Amani Bolugwa.
Katika hafla hiyo Lissu alisema falsafa yake ya No Reform, No Election inaendelea na akawataka wanachama wote kuungana ili uchaguzi ujao uwe huru na haki.
Alipoulizwa na wanahabari kwamba mbona siku zimekwisha Lissu alisema uamuzi wa kuunganisha nchi ya Tanganyika na Zanzibar ulifanywa na Bunge kwa siku moja tun a siku ya Jumamosi, hivyo hakuna sababu ya kushindikana kubadilisha mfumo wa uchaguzi kwa kusingizia muda.
Alisema hakuna haja ya kuingia kwenye uchaguzi huku wakijua kwamba watafanywa washindwe huku akiwakumbusha wanachama wao walivyofanyiwa na CCM katika chaguzi zilizopita.
Akizungumzia uchaguzi wao ndani ya Chadema Lissu alisema: “Sababu iliyofanya tusemezane vibaya imepita, sababu iliyotufanya tuvutane imepita na imepita kwa namna ambayo nchi hii nzima inaisifia.
Nchi nzima hii inatusifia kwa hiyo kwa sababu tumefanya jambo ambalo kila mtu anatusifia bado tuna sababu ya kuvutana? Hapana.
Tunarudi wote nyumbani kwa sababu wote ni wa nyumba moja kwa hiyo baada ya kelele yote hii turudi nyumbani kwetu(CHADEMA) tuangalie palipobomoka tukajenge palipopasuka tuparekebishe wote.”
Na Elvan Stambuli, GPL
0 Comments