Mkoa wa Morogoro watajwa kuwa Kanda Maalum ya ufugaji wenye tija kwa kuwa na ng'ombe wa kisasa na mashamba ya malisho kwa ajili ya mifugo.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amebainisha hayo Januari 03, 2025 katika Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro alipokuwa akizungumza na baadhi ya wafugaji wa mkoa huo akifafanua kuwa nia ya serikali ni kuhakikisha Sekta ya Mifugo inakua na mchango mkubwa katika pato la taifa.
"Kwa sasa Sekta ya Mifugo inachangia chini ya asilimia 10 ambapo nia yetu ni kuhakikisha ifikapo Mwaka 2030 sekta hii inachagia asilimia 10 na kuendelea na hii itatokana na ufugaji wa kisasa na uwepo wa malisho ya uhakika kwa ajili ya mifugo ili kutoa mazao bora yanayotokana na mifugo. " Amesema Mhe. Dkt. Kijaji.
Ameongeza kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi na uongozi wa Mkoa wa Morogoro watahakikisha inawekwa miundombinu ya ufugaji wa kisasa na mbegu bora za mifugo ili kuonesha mfano kwa mikoa mingine huku akiwaasa wafugaji kuwa na tabia ya kushirikiana na serikali katika ujenzi wa miundombinu ya ufugaji.
Aidha, amesema ameridhishwa na utulivu uliopo wa migogoro ya wakulima na wafugaji katika mkoa huo na kutaka kuwepo na elimu zaidi juu ya matumizi bora ya ardhi.
Pia amewataka wafugaji wanaposafisha maeneo kwa ajili ya kulima malisho ya mifugo kutokata miti na kutoharibu vyanzo vya maji ili kutunza mazingira na kuhakikisha uwepo wa visima maeneo ya ufugaji.
0 Comments