MKUU wa Mkoa wa Mtwara Kanali Patrick Sawala amewataka wanafunzi wa kidato cha nne kutoka shule ishirini za sekondari zilizopo katika Manispaa ya Mtwara Mikindani kusoma kwa badii ili kujiandaa na kesho iliyo bora.

Akizungumza mkoani Mtwara wakati wa kongamano la elimu kwa wanafunzi wa kidato cha nne mwaka 2025 lililofanyika katika manispaa hiyo, mkuu huyo wa Mkoa amesema wanafunzi hao wanayo nafasi ya kujirekebisha hasa wale waliyowahi kufanya makosa katika kipindi cha nyuma.

‘’Nawaambie wanangu asiwadanganye mtu yoyote, elimu ya kidato cha nne ina nafasi kubwa sana katika maisha yako, ukifaulu kidato cha nne ndiyo unaweza kuendelea kidato cha tano au ukaendelea chuo hivyo ili kujiandaa na kesho iliyo bora musome kwa bidii’’amesema Sawala.

Hata hivyo amempongeza mkurugenzi wa manispaa hiyo kwa jitihada zake kubwa anazoziweka kwenye manispaa hasa usimamizi wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayogusa sekta tofauti ikiwemo elimu.

Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Mwalimu Hassan Nyange ameahidi kutoa kiasi cha fedha Sh milioni 43.5 kwa shule 11 za serikali za kutwa zilizopo kwenye manispaa hiyo kwa ajili ya mahitaji ya kambi kwa wanafunzi wa kidato cha nne kupitia mfuko wa elimu.

Fedha hizo zitatolewa ikiwa ni moja ya mkakati wa kuweka mazingira mazuri ya kujisomea kwa wanafunzi hao na kujiandaa vema kwenye mtihani wao wa kumaliza elimu ya sekondari ili kuongeza ufaulu na kufuta daraja sifuri.

Shule zitakazohusishwa na mgao wa fedha hizo ikiwemo shule ya sekondari ya Shangani, Rahaleo, Mangamba, Sino Tanzania Friendship, Sabasaba, Naliendele, Umoja, Bandari, Mikindani, Chuno pamoja na Mitengo sekondari.

Kongamano hilo limeandaliwa na manispaa hiyo lengo ni kuhamasisha ufaulu na kuweka mikakati ya kuondoa daraja sifuri na kukutanisha wanafunzi 2,130 wa kidato hicho cha nne kutoka kwenye shule hizo 20 za sekondari zilizopo kwenye manispaa hiyo.

Kongamano hilo linaenda sambamba na kauli mbiu inayosema ‘Ufaulu Manispaa ya Mtwara Mikindani bila daraja o inawezekana’