CONGO: WAASI wa M23 wameendelea kudhibiti sehemu kubwa ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na sasa wameuzunguka mji wa Goma kwa karibu kutoka kila upande.

Rais Felix Tshisekedi, ambaye alikuwa akiendelea na ziara yake nchini Uswisi kuhudhuria Kongamano la Kiuchumi Ulimwenguni mjini Davos, alilazimika kukatiza ziara hiyo na kurejea Kinshasa.

Alirejea Alhamisi, Januari 23, na kuitisha mkutano wa dharura wa usalama kujadili hali mbaya ya vita vinavyoendelea Kivu Kaskazini.

Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi wakuu, akiwemo Waziri Mkuu Judith Suminwa pamoja na mawaziri wa ulinzi na usalama wa taifa.

 

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ikulu ya Kinshasa, Rais Tshisekedi alitarajiwa kuitisha mkutano wa baraza kuu la ulinzi siku ya Ijumaa, Januari 25, utakaofuatiwa na mkutano wa baraza la mawaziri.

Wakatihuohuo,Ubalozi wa Marekani mjini Kinshasa umetoa tahadhari kwa raia wake kuhusu kuongezeka kwa mapigano karibu na mji wa Sake na kuwataka kuwa makini.

Uingereza pia imesema waasi wa M23 wameudhibiti mji wa Sake na kuwaonya raia wake kuondoka Goma huku  Ujerumani imetangaza tahadhari kwa raia wake na kuhimiza kutoenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo isipokuwa kwa ajili ya dharura.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, kupitia msemaji wake Stephane Dujarric, amesikitishwa na kuzuka tena kwa mapigano, akisema mashambulizi hayo yanahatarisha usalama wa raia na kuongeza uwezekano wa vita vya kikanda.

Guterres alitoa wito wa kuachana na ghasia hizo na kutaka waasi wa M23 waondoke katika mji wa Sake, ulio umbali wa kilomita 27 magharibi mwa Goma.

Guterres pia aliunga mkono juhudi za upatanishi zinazofanywa na Rais wa Angola kati ya Rwanda na Congo, akisisitiza umuhimu wa kuheshimu usitishaji mapigano.

Katika kuendeleza juhudi za upatanishi, Rais wa Uturuki, Recep Erdogan, amependekeza kuwa Rwanda na Congo lazima wamalize tofauti zao kwa njia ya mazungumzo.

“Uturuki iko tayari kutoa msaada wowote muhimu ili kutatua mgogoro kati ya Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo,” alisema Erdogan.

Rais wa Uturuki ana mahusiano mazuri na Rais Tshisekedi, ambaye alifanya ziara mbili nchini Uturuki, huku Erdogan alizuru Congo mnamo Februari 2022.

Swali linaloibuka ni kama juhudi hizi za upatanishi zitafanikiwa, hasa kutokana na misimamo mikali ya hivi karibuni kati ya Rais Tshisekedi na Rais Kagame, ambao wamekuwa wakifanya diplomasia ya vitisho na matusi.

Je mgogoro huu utaisha kwa mazungumzo  au lah?