DAR ES SALAAM; WATOTO 19 wamezaliwa katika hospitali za mkoa za rufaa Dar es Salaam usiku wa kuamkia Mwaka Mpya wa 2025.
Maofisa habari wa hospitali hizo walithibitisha hayo jana walipozungumza na HabariLEO.
Kati yao watoto hao, wanane walizaliwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, wanane Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala na watatu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke.
Ofisa Uhusiano wa Hospitali ya Muhimbili Upanga, Angela Mndolwa alisema watoto waliozaliwa Upanga ni wanne, wa kike wawili na wa kiume wawili.
“Wamezaliwa pacha wa kike na kiume kwa njia ya kawaida, ila hao wawili wengine mmoja ambaye ni wa kiume amezaliwa kwa njia ya upasuaji,” alisema Angela.
Alisema wote wanaendelea vizuri kiafya lakini bado hawajaruhusiwa kwenda nyumbani.
Naye Ofisa Uhusiano wa Mloganzila, Priscus Silayo alisema watoto waliozaliwa usiku wa mwaka mpya walikuwa wanne, wa kike wawili na wa kiume wawili. Wote wanaendelea vizuri ila bado hawajaruhusiwa kwenda nyumbani.
Ofisa Uhusiano wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala, Florian Kaijage alisema katika hospitali hiyo walizaliwa watoto wanane, kati yao wa kike mmoja na wa kiume saba.
“Katika hao pia kuna pacha na kuna watatu waliozaliwa kwa upasuaji, yaani hao pacha na mwingine mmoja. Watoto na mama zao wote wanaendelea vizuri kiafya,” alisema Kaijage.
Aidha, katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke walizaliwa watoto watatu, wa kike wawili na wa kiume mmoja.
“Wote wamezaliwa kwa njia ya kawaida na maendeleo yao ni mazuri ingawa bado wapo chini ya uangalizi wa madaktari,” alisema Ofisa uhusiano wa hospitali hiyo, Onesmo Milanzi.
0 Comments