Waziri mkuu wa Thailand Paetongtarn Shinawatra ametangaza mali zenye thamani ya zaidi ya dola milioni 400, chama chake kimesema.

Mali hizo zinajumuisha zaidi ya mikoba ya mkononi 200 iliyotengenezwa na wabunifu yenye thamani ya dola milioni 2 na saa 75 za kifahari zenye thamani ya dola milioni 5.

Paetongtarm, binti mdogo wa bilionea katika sekta ya mawasiliano ya simu na waziri mkuu wa zamani Thaksin Shinawatra, alichukua wadhifa huo Septemba mwaka jana kama mwanachama wa nne wa ukoo huo kuiongoza serikali ya Thailand katika kipindi cha miaka 20.

Paetongtarm alilazimika kutangaza mali na madeni yake Ijumaa iliyopita kwa Tume ya kitaifa ya kupambana na ufisadi (NACC).

Alikiri kuwa na mali zenye thamani ya baht bilioni 13.8, sawa na dola milioni 400, waraka uliochapishwa kwenye tovuti za vyombo vya Habari nchini humo  ulionyesha.