Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Felchesmi Mramba akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Februari 7, 2025 kuhusiana na mkutano wa Afrika Mashariki wa Mafuta na gesi (EAPCE'25) utakaofanyika kituo cha Mikutano cha Julius Nyerere (JINCC) jijini Dar Es Salaam Machi 5 hadi 7, 2025.
Na Avila Kakingo, Michuzi Tv
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa mgeni Rasmi wa mkutano wa Afrika Mashariki wa Mafuta na gesi (EAPCE'25) utakaifanyika katika kituo cha Mikutano cha Julius Nyerere (JINCC) jijini Dar Es Salaam Machi 5 hadi 7, 2025.
Katika Mkutano huo Tanzania itakuwa mwenyeji wa mkutano na Maonesho ya 11 ya Petroli ya Afrika Mashariki (11TH East African Petroleum Conference and Exhibition - EAPCE’25).
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Februari 7, 202, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Felchesmi Mramba amesema kuwa mkutano huo wa EAPCE’25 utatoa nafasi ya kujadili mchango wa rasilimali za mafuta na gesi asilia katika mchanganyiko wa nishati kwa maendeleo endelevu ya Afrika Mashariki na fursa za uwekezaji zilizopo katika sekta ya mafuta na gesi Afrika Mashariki.
Aidha, Mhandisi Mramba ameeleza kuwa mada mbalimbali kutoka kwa wataalam na wabobezi katika sekta ya mafuta na gesi zitatolewa zikiwemo utafutaji na uendelezaji wa mafuta na gesi katika nchi za Afrika Mashariki, fursa za uwekezaji katika mnyororo wa thamani wa mafuta na gesi, dhana ya kuelekea nishati safi, masuala ya mazingira, miundo ya kisera, kisheria na kiudhibiti katika mafuta na gesi na kadhalika.
"Mkutano utahusisha maonesho ya bidhaa na huduma kutoka kampuni mbalimbali katika mnyororo wa thamani wa mafuta na gesi asilia." Amesema
Aidha, Mramba amesema kuwa Mkutano wa EAPCE’25 unafanyika katika wakati muhimu baada ya Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika kujadilia masuala ya nishati.
"Katika mkutano wa Mission 300 nchi za Afrika zilikubaliana kuweka Mpango Mahususi wa Taifa wa Nishati kwa kipindi cha miaka mitano 2025-2030 ambapo kwa Tanzania mpango wetu ni kuunganisha watumiaji wa umeme kufikia 75%, kuongeza kiwango cha upatikanaji umeme kufikia 100% na kuwezesha matumizi ya nishati safi ya kupikia kufikia 75% ifikapo mwaka 2030."
"Ili kufikia malengo haya tunahitaji kutumia rasilimali zetu za asili ikiwemo za mafuta na gesi ili kuchangia katika upatikanaji wa nishati ya uhakika ikiwemo nishati safi ya kupikia.”Mramba amesema
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kikanda ya maandalizi ya EAPCE’25 ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi, Dkt. James Mataragio ameongeza kuwa Mkutano huo unahusisha pia ziara za kitaaluma katika maeneo ya kijiolojia katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kuwapa washiriki mtazamo wa vitendo kuhusu sekta.
Dkt. Mataragio amesema “Ziara hizi zitatoa fursa ya kuona miradi inayoendelea na mipango ya baadaye, jiolojia katika nchi za Afrika Mashariki na hivyo kuwawezesha wawekezaji na wadau kubaini fursa za biashara na ushirikiano katika sekta ya nishati katika ukanda wetu.”
Kuhusu utaratibu wa kushiriki katika mkutano wa EAPCE’25, Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Maandalizi, Mhandisi Joyce Kisamo amesema “Tunawahimiza makampuni na wadau mbalimbali wa sekta ya mafuta na gesi kujiandikisha kushiriki katika mkutano huu na pia kutumia nafasi hii kutangaza bidhaa na huduma zao kupitia maonesho”.
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) inajumuisha nchi wanachama wanane Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini, Somalia, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Kauli mbiu ya Mkutano huo itakuwa, ni “Kufungua Fursa za Uwekezaji katika Nishati Mchango wa Rasilimali za Mafuta katika Kupata Nishati ya Uhakika kwa Maendeleo Endelevu ya Afrika Mashariki.”
Mkutano huo utatanguliwa na semina kuhusu masuala ya nishati safi ikiwemo nishati safi ya kupikia na matumizi ya gesi kwenye magari (CNG) itakayofanyika tarehe 4 Machi, 2025.
Mkutano wa EAPCE’25 utawaleta pamoja washiriki zaidi ya 1000, wakiwemo watunga sera, viongozi wa Serikali kutoka nchi mbalimbali ikiwemo nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, wawekezaji wa kimataifa na wa ndani.
Kwa taarifa zaidi kuhusu Mkutano wa EAPCE’25 pamoja na kujisajili kushiriki, tafadhali tembelea www.eapce25.eac.int au mitandao ya kijamii kama mtandao wa X na Instagram kwa jina la: @eapce25.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kikanda ya maandalizi ya EAPCE’25 ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi, Dkt. James Mataragio akizungumza wakati wa kutambulisha mkutano wa Mafuta na Gesi wa Afrika Mashariki utaofanyika jijini Dar es Salaam Machi 5-7, 2025.
.jpeg)
Picha ya Pamoja.
0 Comments