Katibu wa NEC, Itikadi, Mafunzo na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) CPA Amos Makalla ameeleza masikitiko yake juu ya tukio la kupigwa kwa Katibu Mwenezi wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), Sigrada Mligo ,34, hatua iliyowatia simanzi na hivyo kumchangia zaidi ya Sh milioni 1.5 kusaidia matibabu.

Katika kuonesha mshikamano wa kijamii, Mjumbe wa Halmshauri Kuu ya CCM Taifa, Salim Asas, amechangia Sh milioni 1 huku wanachama na wafuasi wengine wa wilaya ya Mufindi wakichangia zaidi Sh 500,000.

Kiongozi huyo wa Bawacha anadaiwa kupigwa na mlinzi wa Makamu Mwenyekiti wa Chadema, John Heche hivi karibuni wakati wa ziara yake ya kichama mkoani Njombe.

Tukio hilo limeelezwa kusababisha majeraha makubwa kwa Mligo jambo lililosababisha alazwe kwa matibabu katika hospitali ya Kibena, mjini Njombe.

Akihutubia wafuasi na wanachama wa CCM mjini Mafinga katika ziara yake aliyoanza leo mkoani Iringa, CPA Makalla aliendesha harambee ya kumchangia kiongozi huyo wa Chadema na kusema chama chao hakitasimama kimya dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia.

“Tunamtakia uponyaji wa haraka Sigrada Mligo, na tunahimiza viongozi wa Chadema kuwa mstari wa mbele kulaani vitendo vya unyanyasaji ndani ya chama chao,” alisema Makalla, ambaye pia amepewa uchifu na wazee wa kimila wa Kihehe na kupewa jina jipya la Mwalamnila Mlongahilo, likimaanisha msema kweli.

 Akiikosoa Chadema na kauli yake ya No Reforms No Election, Makalla alizungumzia namna Serikali ya Dk Samia Suluhu Hassan ilivyoyafanyia kazi maombi ya wadau wa siasa kuhusu sheria za uchaguzi.

Alisema kwa kupitia Bunge, sheria inayounda Tume Huru ya Uchaguzi na inayozuia wakurugenzi wa halamshauri kuwa wasimamizi wa uchaguzi kwa ngazi ya majimbo imeundwa.

Wakati Chadema wakipotosha umma kuhusu sheria hiyo, mwenezi huyo wa CCM alifafanua kwamba sheria hiyo imeweka utaratibu wa namna viongozi na wajumbe wa tume hiyo huru ya uchaguzi watakavyopatikana kupitia tume maalumu itakayoongozwa na Jaji Mkuu.

“Sheria hiyo inatoa mwongozo wa wazi kuhusu namna ya kuteua wajumbe wa tume hiyo, ambapo maombi yatafanyika kwa njia rasmi na kupelekwa kwa chombo hocho kitakachoongozwa na jaji mkuu kwa uchambuzi wa kina” alisema.

Aidha alisema sheria ya uchaguzi sasa inahakikisha kuwa hakuna kiongozi wa kuchaguliwa atakayepita bila kupingwa na wakurugenzi wa halmashauri hawatakuwa wasimamizi wa uchaguzi tena, badala yake kazi hiyo itafanywa na maafisa waandamizi wa umma.

CPA Makalla pia ameweka wazi kuwa CCM itaendelea kushiriki uchaguzi kwa mujibu wa Katiba, huku akiwahimiza wananchi kuendelea kuiamini na kuiunga mkono ili iendelee kupata ushindi wa kishindo katika kata, majimbo, na urais.

“Mkoa wa Iringa, hususan Wilaya ya Mufindi, ni ngome imara ya CCM. Pamoja na maneno mengi yanayotolewa na wapinzani, ukweli ni kwamba CCM imetekeleza miradi mingi ya maendeleo, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu, huduma za afya, elimu, na maji safi,” alisema. Aliwashangaa wanaobeza maendeleo yanayofanywa na serikali ya CCM na kuwafananisha vipofu wanaohitaji kusaidiwa kuona.

Aidha CPA Makalla ameonya vikali juu ya msimamo wa Chadema wa kususia uchaguzi, akieleza kuwa hatua hiyo ni kinyume na Katiba na inalenga kuficha udhaifu wa chama hicho katika maandalizi ya uchaguzi.

“Hakuna sheria inayosema kuwa uchaguzi unasitishwa kwa sababu chama fulani hakijajiandaa. CCM itaendelea na maandalizi ya uchaguzi bila kujali msimamo wa Chadema,” alisema.

Aliongeza kuwa mikakati ya Chadema ya kuzuia uchaguzi haina mashiko, kwani vyama vingine viko tayari kushiriki, na hata wanachama wa Chadema wenye nia ya kugombea wanaweza kuhamia vyama vingine kama vile CCM ili kutimiza ndoto zao za uongozi.

Katika hatua nyingine, CPA Makalla alitangaza kuwa CCM itaendesha kampeni zake kwa mujibu wa misingi ya kistaarabu, huku ikijikita katika sera na utekelezaji wa Ilani yake badala ya matusi na uchochezi.