Joshlin Smith hajapatikana hadi sasa, zaidi ya mwaka mmoja baada ya kutoweka

Mama wa binti wa miaka sita kutoka Afrika Kusini, ambaye alitoweka zaidi ya mwaka mmoja uliopita, amepatikana na hatia ya kumteka na kumsafirisha binti yake.

Mama huyo aitwaye Kelly Smith, mpenzi wake Jacquen Appollis na rafiki yao Steveno van Rhyn walikamatwa baada ya binti wa Kelly, aitwaye Joshlin, kutoweka huko Saldanha Bay, karibu na Cape Town, Februari mwaka jana.

Appollis na Rhyn pia wamepatikana na hatia siku ya Ijumaa ya kumteka nyara na kumsafirisha Joshlin. Wote watatu hapo awali walikana mashtaka haya.

Kutoweka kwa Joshlin kulileta mshtuko kote Afrika Kusini na licha ya kutafutwa na kutangazwa kwa umma, bado mtoto huyo hajapatikana.

Wakati wa kesi hiyo, iliyofanyika Machi, waendesha mashtaka walimshtaki Kelly kwa "kumuuza, kumsafirisha au kumbadilishana" Joshlin na kisha kudanganya kuhusu kutoweka kwake.

Huku Waafrika Kusini wakimsubiri Jaji Nathan Erasmus kutoa uamuzi wake siku ya Ijumaa, kuna watu wengi nje ya jengo la mahakama ya ya Saldanha Multipurpose Centre.

Barabara za karibu zimefungwa kwa kutarajia idadi kubwa ya watu watakaojitokeza, huku maafisa wa polisi wakiwekwa ndani na nje ya kituo hicho.

fc

CHANZO CHA PICHA,GALLO IMAGES

Maelezo ya picha,Kutoka kulia Jacquen Appollis, Steveno van Rhyn na Kelly Smith wakati wa kesi ya Joshlin Smith

Kesi ya Smith iliteka vichwa vya habari Afrika Kusini, huku mashahidi na waendesha mashtaka wakitoa madai kadhaa ya kutisha.

Madai ya kutisha zaidi yalitoka kwa Lourentia Lombaard, rafiki na jirani wa Kelly ambaye aligeuka kuwa shahidi wa serikali.

Bi Lombaard alidai kuwa Kelly alimwambia kuwa amefanya "kitu cha kijinga" na kumuuza Joshlin kwa mganga wa kienyeji, anayejulikana nchini Afrika Kusini kama "sangoma".

"Mtu ambaye [anayedaiwa kumchukua] Joshlin alimtaka binti huyo kwa sababu ya macho na ngozi yake," Bi Lombaard aliambia mahakama.

Mchungaji wa eneo hilo alitoa ushahidi kwamba mwaka 2023, alimsikia Kelly - mama wa watoto watatu – akizungumzia juu ya kuwauza watoto wake kwa randi 20,000 (dola za kimarekani 1,100; £850) kila mmoja, ingawa alisema yuko tayari kukubali kiwango cha chini cha dola 275.