SINGIDA: WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete, ameeleza kuwa ndani ya miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan wafanyakazi 412,000 wamepandishwa madaraja na kulipwa stahiki zao katika sekta ya umma.

Ridhiwani amebainisha mafanikio hayo leo Mei Mosi, 2025 wakati wa sherehe za siku ya wafanyakazi duniani, zinazofanyika kitaifa mkoani Singida kwenye viwanja vya bombadia, akieleza kuwa ndani ya miaka minne ya Rais Samia Suluhu, wafanyakazi wa umma wameongezewa Posho kwa asilimia mia moja ili kuweza kumudu gharama mbalimbali za maisha.

“Umeelekeza pia malipo ya mkupuo Mhe Rais, kwa furaha kubwa nikuhakikishie jambo hilo limefanyika kupitia mifumo iliyowekwa na sekta binafsi na ya umma malipo ya mikupuo yamefanyika na jambo la uungwana ulilofanya wale walioondolewa kwenye vyeti feki umekubali walipwe asilimia tano ya mafao yao. Huu ni uungwana, ni ubinadamu na Upendo mkubwa sana kwa wafanyakazi,” amesema Ridhiwani.

Aidha Katika hatua nyingine, Ridhiwani amemshukuru Rais Samia kwa maamuzi yake ya kuamua kuwa serikali kuu ilipe mishahara kwa watumishi walio kwenye Halmashauri zinazosuasua katika mishahara, akieleza kuwa kwasasa Halmshauri zaidi ya 58 wafanyakazi wake wanalipwa mishahara na serikali kuu.

Akizungumzia kaulimbiu ya mwaka huu isemayo, ‘Uchaguzi Mkuu 2025, utuletee viongozi wanaojali haki na maslahi ya wafanyakazi, sote tushiriki’

Ridhiwani amesema kaulimbiu hiyo inaakisi jitihada zinazofanywa na Rais Samia kwa watumishi wa Tanzania na hivyo kutoa urahisi kwa wasaidizi wake.