Umoja wa Ulaya (EU) na Mexico zimeelezea kusikitishwa na tishio la Rais wa Marekani Donald Trump la kutoza ushuru wa asilimia 30 kwa bidhaa zinazotoka nje kuanzia tarehe 1 Agosti.
Mexico ilikosoa kile ilichokiita "mkataba usio wa haki" wa Trump na kusisitiza uhuru wake hauwezi kujadiliwa, wakati mkuu wa EU, Ursula von der Leyen akitishia kuchukua "hatua sawia", ikiwa itahitajika. Wote wawili walisema wanataka kuendelea kufanya mazungumzo na Marekani.
Trump ameonya kuwa atatoza ushuru mkubwa zaidi wa bidhaa kutoka nje ikiwa mmoja wa washirika wa biashara wa Marekani wataamua kulipiza kisasi.
Wiki hii Trump pia alitangaza ushuru mpya kwa bidhaa kwa Japan, Korea Kusini, Canada na Brazil kuanzia mwezi ujao.
Katika barua iliyotumwa siku ya Ijumaa kwa Rais wa Tume ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen, Trump aliandika: "Tumekuwa na miaka ya kujadili uhusiano wetu wa kibiashara na Umoja wa Ulaya, na tumehitimisha kwamba lazima tuondokane na upungufu huu wa muda mrefu, na unaoendelea wa biashara, unaosababishwa na ushuru wako, na usio wa ushuru, sera na vikwazo vya biashara."
''Uhusiano wetu umekuwa, kwa bahati mbaya, mbali na maelewano," barua hiyo iliongeza.
Katika barua zake kwa Umoja wa Ulaya na Mexico, Trump alionya kwamba iwapo mshirika wa kibiashara atalipiza kisasi ushuru wake dhidi ya Marekani, atajibiwa kwa kuongeza ushuru kwa asilimia zaidi ya 30.

0 Comments