Hospitali ya Nasser kusini mwa Gaza imesema watu 24 wameuawa karibu na eneo la kusambaza misaada.
Wapalestina waliokuwepo katika eneo hilo walisema wanajeshi wa Israel walifyatulia risasi watu walipokuwa wakijaribu kupata chakula siku ya Jumamosi.
Jeshi la Ulinzi la Israeli (IDF) lilisema "hakuna watu wanaojulikana waliojeruhiwa" kutokana na moto wa IDF karibu na eneo hilo.
Kando na hilo, afisa wa kijeshi wa Israel alisema risasi za onyo zilipigwa ili kuwatawanya watu ambao IDF iliamini kuwa ni tishio.
Madai ya pande zote mbili hayajathibitishwa. Israel hairuhusu mashirika ya habari ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na BBC, kuingia Gaza.
Picha zilizoonekana na BBC baadaye Jumamosi zilionesha kile kilichoonekana kuwa idadi ya mifuko ya miili katika ua wa hospitali ya Nasser ikiwa imezungukwa na wauguzi na watu waliovalia nguo zilizotapakaa damu.
Katika video nyingine, mwanaume mmoja alisema watu walikuwa wakingoja kupata usaidizi walipofyatuliwa risasi kwa dakika tano.
Video hizo hazijathibitishwa na BBC. Reuters ilisema ilizungumza na mashahidi ambao walielezea watu kupigwa risasi kichwani.
Shirika la habari pia liliripoti kuona miili imefungwa kwa sanda nyeupe katika hospitali ya Nasser.
Kumekuwa na ripoti karibu kila siku za watu kuuawa na Israel walipokuwa wakitafuta chakula huko Gaza.

0 Comments