Luhaga Mpina ameshinda shauri la kupinga kuenguliwa kugombea urais wa Tanzania kwa tikiti ya ACT Wazalendo.

Uamuzi huo umetolewa na majaji watatu wa Mahakama Kuu ya Tanzania jijini Dodoma muda mfupi uliopita.

Mamia ya wafuasi na wasio wafuasi wa Chama ACT Wazalendo walikuwepo katika Mahakama Kuu, Masijala kuu ya Dodoma kufuatilia uamuzi wa shauri la Luhaga Mpina.

Baadhi ya wanasiasa mashuhuri akiwemo kiongozi mkuu wa zamani wa ACT, Zitto Kabwe ni miongoni mwa waliofika kufuatilia uamuzi wa shauri lililofunguliwa na ACT Wazalendo dhidi ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi nchini Tanzania.

Shauri hilo ambalo lilifunguliwa na bodi ya wadhamani ya ACT Wazalendo na mgombea mteule wa kiti cha urais kupitia chama hicho lilipinga kuondolewa kwa Mpina kwenye mchakato wa uchaguzi Mkuu kwa kuzuiwa kurejesha fomu ya kuomba uteuzi wa kugombea nafasi ya urais.

Shauri hili ambalo lilifunguliwa kwa hati ya dharura lilisikilizwa na jopo la majaji watatu likiongozwa na Abdi Kagomba, Evaristo Longopa na John Kahyoza.