Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi inasema Poland imekuwa ikieneza "simulizi za uwongo" kuhusu uvamizi wa ndege zisizo na rubani ili "kuzidisha mzozo wa Ukraine".

Katika taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti yake, wizara ya mambo ya nje inakariri kwamba haikuwa imepanga kulenga eneo la Poland.

"Ukweli huu halisi unaondoa kabisa simulizi za uongo zilizoenezwa tena na Poland ili kuzidisha mzozo wa Ukraine," wizara hiyo inasema.

Inaongeza kuwa Katibu Mkuu wa Nato Mark Rutte "hakuweza kujibu swali kama kulikuwa na ushahidi wowote" wa shambulio lililopangwa.

Wakati huo huo, waziri wa Poland Tomasz Siemoniak aliishutumu Urusi kwa kueneza habari potofu kuhusu uvamizi wa ndege zisizo na rubani. Alichapisha kwenye X, kwamba Urusi imezindua "kampeni kubwa ya upotoshaji" na kwamba "ilikuwa ikiikashifu Poland."

Poland imeungwa mkono kikamilifu na washirika wake wa Nato, ambao wamelaani uvamizi wa ndege zisizo na rubani katika eneo la Poland.