Idadi ya watu walionyongwa nchini Iran mwaka 2025 inakadiriwa kuwa zaidi ya mara mbili ikilinganishwa na idadi ya hukuma iliyotekelezwa kote nchini mwaka 2024.
Kundi la Haki za Kibinadamu la Iran (IHR) lenye makao yake makuu nchini Norway (IHR) liliiambia BBC kuwa limethibitisha angalau watu 1,500 walionyongwa hadi mwanzoni mwa Desemba, na kuongeza kuwa wengi zaidi wametekelezwa tangu wakati huo. Mwaka jana, IHR iliweza kuthibitisha watu 975 walionyongwa - ingawa idadi kamili haiko wazi kabisa kwani mamlaka ya Irani haitoi takwimu rasmi.
Hata hivyo, uchambuzi unaonyesha ongezeko lingine kubwa la kila mwaka, na takwimu zinalingana na zile zinazotolewa na vikundi vingine vya ufuatiliaji.
Serikali ya Iran hapo awali ilitetea utumiaji wake wa adhabu ya kifo, ikisema kuwa inahusu tu "uhalifu mbaya zaidi".
Takwimu za kunyongwa tayari zilikuwa zimeongezeka kabla ya maandamano makubwa yaliyozuka kote nchini humo mwaka 2022 kufuatia kifo cha Mahsa Amini. Mwanamke huyo wa Kikurdi mwenye umri wa miaka 22 alizuiliwa na polisi wa maadili mjini Tehran kwa madai ya kuvaa hijabu yake "isivyofaa".

0 Comments