MKUU wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka amewataka vijana kulinda amani ya Tanzania kwani wao ndiyo wanabeba matumaini ya taifa.

Aliyasema hayo juzi alipokuwa akizungumza katika ibada katika Kanisa la Wadventista Wasabato, Njombe mjini.

“Vijana wetu wa Gen Z wana wajibu wa kulinda amani ya Tanzania, ninyi ndiyo kizazi kinachobeba matumaini na sura ya taifa letu,” alisema Mtaka.

Alisema amani ni tunda la haki na wajibu na msingi thabiti wa maendeleo kwenye jamii na wananchi wana wajibu wa kuilinda amani ya nchi kwa wivu mkubwa na kwamba vijana wa leo wanapaswa kuitunza amani kwa faida ya vizazi vilivyopo na vijavyo waikute Tanzania iliyo moja.

 

Aliwahakikishia wananchi wa Njombe kuwa mkoa huo uko salama na hauna matishio ya kihalifu na kwamba wanaendelea kujenga mazingira thabiti ya ulinzi wa watu na mali ili kutoa fursa kwa wananchi kuendelea kufanya shughuli zao za uzalishaji mali na mahangaiko yao ya kujipatia kipato cha siku.

“Usalama wa mkoa wetu utatuongezea imani kwa wawekezaji wetu mbalimbali kuendelea kuamini kwamba Njombe ni mahali sahihi pa wao kuweka mitaji yao, wana Njombe tushikamane kuhakikisha tunaziepuka aina zozote za chokochoko zitakazoashiria uhalibifu wa mali, uwekezaji, miradi ya umma na binafsi au uharibifu wa uhai wa wananchi wenzetu,” alisema.

Alisema endapo wananchi wataona au kuhisi dalili yoyote inayoashiria uvunjifu wa amani au kuhatarisha usalama wa maeneo yao au maisha ya mtu, watoe taarifa mapema kwa kuwa ulinzi shirikishi huanza na wanajamii kutoa taarifa kwa wakati.