DAR ES SALAAM:Waziri wa Afya ,Mohammed Mchengerwa amesema kuwa viwango vya ubora wa utengenezaji dawa kimataifa lazima vifikiwe.

Kutokana na hali hiyo amesisitiza kuwa serikali itafanya kazi kwa karibu na watengenezaji dawa ili kufikia viwango hivyo.

Amesema hayo jijini Dar es Salaam wakati wa Kongamano la wazalishaji dawa pamoja na  vifaatiba na kueleza kuwa wawekezaji wengi wamejengaa viwanda,  lakini taratibu za kimataifa walikuwa hawajaanza.

Amesema wanataka kila  mwekezaji aweze kupata hati inayomtambua kimataifa kuwa na viwango vya ubora wa dawa, kwani eneo la dawa ni  nyeti si la majaribio.

“Ukifanya kuwa eneo la majaribio unaweza kuangamiza Watanzania walio wengi, hatuwezi kuruhusu hata kidogo, tunataka wawekezaji wa ndani ambao bado hawajapata hati za viwango vya kimataifa waanze mchakato,” amesema.
 
Amesema maofisa wa wizara wako karibu nao na wadau wa masuala hayo, ili kuwapa taratibu kuwasaidia na kuwakwamua pale ambapo kuna changamoto.

Ametoa onyo kwa yeyote anayejaribu kuingilia mchakato huo hata kwa  waagizaji wa nje, kwani watapambana nao na kuwa maamuzi hayo ni ya Rais Samia Suluhu Hassan,  hivyo hatakuwepo wa kupinga watasimama na wawekezaji wa ndani kujenga viwanda ndani.

Amesema watahakikisha mazingira ya uwekezaji wa dawa,vifaatiba na chanjo yanakuwa   ni rahisi hapa nchini.