Wanafunzi 13 wamefariki dunia nchini Afrika Kusini baada ya basi dogo walilokuwa wakisafiria kugongana na lori kusini mwa jiji la Johannesburg.

Ajali hiyo ilitokea Jumatatu asubuhi majira ya saa 1:00 kwa saa za huko (05:00 GMT) katika eneo la Vanderbijlpark, kwa mujibu wa mamlaka ya elimu ya eneo hilo.

Wanafunzi 11 walifariki papo hapo katika eneo la ajali, huku wawili wakifariki baadaye kutokana na majeraha waliyoyapata.

Wanafunzi wengine wawili wameripotiwa kuwa katika hali mbaya mahututi.

Kwa mujibu wa msemaji wa polisi, Mavela Masondo, dereva wa basi hilo amesema aligonga lori baada ya kujaribu kupita magari mawili kwa wakati mmoja.

Masondo aliongeza kuwa kesi ya mauaji yasiyokusudiwa itafunguliwa kuhusiana na ajali hiyo.

Idara ya elimu ya mkoa wa Gauteng imesema dereva wa basi dogo anapatiwa matibabu hospitalini, huku taarifa kuhusu hali ya dereva wa lori zikiwa bado hazijabainika.

Ajali za barabarani zinazosababisha vifo ni za kawaida nchini Afrika Kusini, kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo mwendo wa kasi kupita kiasi, uendeshaji hatarishi wa magari na magari yasiyotunzwa ipasavyo.

Mwaka 2025, watu 11,418 walifariki kutokana na ajali za barabarani, idadi ambayo ni pungufu kwa takribani asilimia 6 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia, lakini bado ni sawa na wastani wa vifo 31 kwa siku.