
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi ameonya watu wanaotumika kuichafua nchi. Katambi amesema hayo kwenye mkutano wa hadhara aliouandaa kushukuru wananchi kumpa ridhaa ya kuwa mbunge wa Shinyanga Mjini.
Amesema Tanzania itaendelea kuwa na amani na utulivu na watu wasione raha kuchukua nakala au picha za mjongeo ambazo zina viashiria vya uvunjifu wa amani na kuendelea kufurahia kuzisambaza kwenye mitandao ya kijamii na kuhatarisha usalama wa nchi.
Katambi amesema amani ikivurugika kuirudisha ni kazi, hivyo wananchi waendelee kuishi kwa amani na upendo bila ubaguzi. Pia amesema watumishi wa serikali ambao hawatekelezi maagizo ya serikali mwisho wake umefika kwani fedha zimekuwa zikitolewa na serikali kwa ajili ya utekelezaji miradi mbalimbali lakini wanachelewesha kwa uzembe wao.
Katambi amesema wananchi wa mjini Shinyanga wameendelea kumuamini hivyo atahakikisha maendeleo yanapatikana kwa kuwa serikali imetoa zaidi ya Sh bilioni 45 kwa ajili ya ujenzi wa kiwanja cha ndege cha Ibadakuli. SOMA: Vikosi vya ulinzi vyajizatiti kulinda amani nchini
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Janeti Magomi amesema hali ya ulinzi na usalama mkoani humo ni shwari. Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa amesema wana imani kwa serikali. Alimuomba waziri Katambi vitambulisho vya taifa (NIDA) vifikishwe kwenye kata ili kuwaondolea wananchi usumbufu.
0 Comments