Mfanyakazi wa nyumbani Vicky Ajok (kushoto) na mwigizaji Huda Shaarawi (kulia)
Serikali ya Uganda iko chini ya shinikizo la kuingilia kati kesi ya mfanyakazi wa ndani anayekabiliwa na adhabu ya kifo nchini Syria.
Shirika la habari la MMI News lenye makao yake Uingereza likinukuu shirika la Migrant Workers Voice Uganda likiwahimiza maafisa jijini Kampala kuzungumza na wenzao wa Syria ili kusimamisha utekelezaji wa hukumu hiyo dhidi ya Vicky Ajok ambayo imepangwa kufanyika mwishoni mwa wiki hii tarehe 28 Februari.
Ajok alihukumiwa kwa kumuua mwajiri wake mwenye umri wa miaka 87, Huda Shaarawi, ambaye ni mwigizaji wa tamthilia maarufu ya televisheni nchini Syria ya Bab Al Hara.
Tukio hilo lilitokea mwezi uliopita katika mji mkuu wa Syria, Damascus.
Kulingana na ripoti, Ajok alimpiga mwajiri wake kwa kitu kizito wakati wa mabishano, na kusababisha majeraha mabaya. Inasemekana alikimbia eneo la tukio lakini baadaye akakamatwa.
Katika taarifa ya kukiri ambayo ilisambazwa katika vyombo vya habari vya ndani, inasemekana alitaja unyanyasaji wa muda mrefu na mishahara isiyolipwa kama sababu zilizosababisha tukio hilo.
Video iliyochapishwa kwenye chaneli ya Uganda ya New Vision YouTube inamwonyesha Ajok akiwa katika chumba akiwa amezungukwa na watu wanaoaminika kuwa maafisa wa Syria, akionyesha jinsi alivyofanya shambulio hilo kabla ya kulia na kuomba msamaha.
Serikali ya Uganda bado haijatoa kauli kuhusu jambo hilo.

0 Comments