Clinton Mogesa, 29, alifariki alipokuwa akipigania Urusi
Jumla ya Wakenya 1,000 wamesajiliwa kupigania Urusi, kulingana na ripoti ya kijasusi ya Kenya ambayo inaeleza mtandao wa maafisa wahalifu wanaodaiwa kushirikiana na makundi ya magendo ya binadamu.
Ripoti hiyo, iliyowasilishwa bungeni siku ya Jumatano na Huduma ya Kitaifa ya Ujasusi ya Kenya (NIS), ilisema Wakenya 89 walikuwa mstari wa mbele katika vita vya Urusi na Ukraine kufikia Februari mwaka huu.
Mkenya mmoja tayari amefariki, huku wengine kadhaa wakirejea nyumbani wakiwa wamejeruhiwa au wakiwa na wasiwasi.
Serikali ya Kenya, ambayo hapo awali ilikadiria kuwa takriban raia wake 200 walikuwa wameajiriwa kupigania Urusi, inataka Moscow kuzuia kuandikishwa kwa raia wa Kenya katika jeshi la Urusi.
Akiwasilisha ripoti hiyo kwa wabunge, kiongozi wa wengi bungeni Kimani Ichung'wah, alifichua kile alichokiita mtandao "unaosumbua sana" wa maafisa wa serikali walaghai wanaodaiwa kushirikiana na makundi ya magendo ya binadamu kuwaajiri na kuwasafirisha Wakenya kupigana katika vita vya Urusi na Ukraine.
Shirika hilo la kijasusi lilieleza kwa kina jinsi mashirika ya kuajiri yamekuwa yakishirikiana na wafanyikazi walaghai wa uwanja wa ndege wa Kenya, maafisa wa uhamiaji, maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI), maafisa wa kupambana na mihadarati na maafisa wa Mamlaka ya Kitaifa ya Ajira ili kurahisisha usafiri wa waajiriwa.
Ichung'wah alidai kuwa mashirika hayo pia yamekuwa yakishirikiana na wafanyikazi katika ubalozi wa Urusi mjini Nairobi na ubalozi wa Kenya mjini Moscow kusaidia waajiri kupata visa za Urusi.
Katika taarifa yake siku ya Alhamisi, ubalozi wa Urusi mjini Nairobi ulipuuzilia mbali madai hayo na kusema ni "hatari na ya kupotosha", ukisema kuwa wafanyakazi wake hawajawahi kuhusika na "mipango ya uhuni" au kujihusisha na usajili haramu.

0 Comments