DAR ES SALAAM: LICHA ya Yanga SC kuwa na baadhi ya wachezaji majeruhi, ila mchambuzi maarufu wa michezo, Ansibert Rafael ‘Hans Rafael’ anaamini utendaji wa timu haujaathirika kwani kocha msaidizi Abdihamid Moalin amerejesha chachu benchi la ufundi.

Mshambuliaji, Laurindo Depu na Clement Mzie ni majeruhi, beki Dickson Job majeruhi, pia Prince Dube alikosekana kwa wiki kadhaa na kurejea mchezo dhidi ya TMA Stars kombe la CRDB.

Akizungumza na HabariLeo mapema leo Aprili 15, 2026, Hans Rafael amesema kwenye mchezo dhidi ya Pamba Jiji, Yanga SC walionesha mabadiliko makubwa ya kimbinu kwa kucheza na viungo wanne na kubadilisha wachezaji maeneo tofauti.

“Wachezaji wa Yanga SC wamekuwa na uchu wa mafanikio, na hii imeanza kwa uongozi wa Injia Hersi Said, amekuwa chachu kubwa sana amekuwa akibeba maono ya klabu,” amesema Hans Rafael.

Aidha, Hans Rafael alimtaja Allan Okello na Mohammed Hussein kuwa ndio usajili mpya ambao una uhakika wa kuanza ndani ya Yanga SC.

“Wengine wamekuwa wachezaji wa kikosi, pia wengi walisajiliwa Julai mwaka jana hawapo msimu huu, hivyo hakuna usajili uliobadili mfumo wa Yanga SC,” amesema Hans Rafael.

Pia Hans aliwasifu wachezaji hao kuwa wameonesha ubora mkubwa kwa wachezaji wapya, hasa katika kutengeneza nafasi za mabao na kufunga pia.

“Allan Okello ameonesha ubora wake akicheza nyuma ya mshambuliaji anakuwa hatari zaidi kuliko akicheza winga ya kulia,” amesema Hans Rafael.

Hans Rafael pia amewasifu Yanga SC kwa kuwa na kikosi kipana chenye ubora kwani wapo wachezaji ambao wanaaminiwa na kucheza kwa ubora.

“Aziz Andambwile ana uwezo wa kuanza Simba SC, leo Mudathir Yahya, Shandrack Boka wana uwezo wa kuanza Simba SC, Mshery ni mjadala dhidi ya Kassali,” ameongeza Hans.

Kwa upande mwingine, Hans Rafael amezungumzia nafasi za makocha wazawa na kigeni, akidai kuwa bila kujali hilo, makocha wote wanapaswa kupewa nafasi.

Amesema changamoto ya wazawa hawana uzoefu wa soka la nje ya Tanzania, pia wengi wao wameridhika na kuwa makocha wa timu za ligi kuu.

“Hawachukui changamoto kutoka nje ya mipaka ya Tanzania, inaleta shida kwa sababu ligi ya Tanzania ina wachezaji wengi wageni hawajui jinsi ya kuwamudu,” amesema Hans Rafael.