Jeshi la Marekani limetangaza kuwa limefanya mashambulizi mengine ya anga dhidi ya malengo kadhaa nchini Iran kwa maelekezo ya Rais Donald Trump.

Kupitia taarifa iliyochapishwa kwenye mitandao ya kijamii, Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) imesema Iran ilipewa nafasi ya kuheshimu makubaliano ya kusitisha mapigano, lakini ilichagua kuyakiuka baada ya kushambulia meli ya kibiashara katika Mlango wa Bahari wa Hormuz mapema Jumamosi.

CENTCOM imeeleza kuwa mashambulizi hayo yalikuwa jibu la moja kwa moja kwa kile ilichokiita kuendelea kwa Iran kushambulia meli za biashara zinazopita katika eneo hilo.

Kwa mujibu wa jeshi hilo, ndege za kivita za Marekani zililenga miundombinu ya ufuatiliaji wa kijeshi, mifumo ya mawasiliano, maeneo ya ulinzi wa anga, maghala ya kuhifadhi ndege zisizo na rubani (drones) pamoja na uwezo wa Iran wa kutega mabomu ya baharini.

Baadaye, Afisa mmoja wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani alinukuliwa na Fox News akisema operesheni ya mashambulizi dhidi ya malengo ya Iran ilikuwa imekamilika.

Nchini Iran, Shirika la Utangazaji la Taifa (IRIB) liliripoti mapema Jumapili kuwa milipuko ilisikika katika mji wa Sirik, kusini mwa nchi, bila kutoa maelezo zaidi kuhusu chanzo chake.

Mashambulizi hayo yanajiri baada ya Marekani kufanya operesheni nyingine kufuatia shambulio la drone la Iran dhidi ya meli ya mizigo iliyokuwa imebeba zaidi ya mapipa milioni mbili ya mafuta ghafi na iliyokuwa ikijaribu kuvuka Mlango wa Hormuz, hali ambayo imeendelea kuongeza mvutano licha ya makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa wiki mbili zilizopita.

Marekani na Iran zimeendelea kutuhumiana kwa kukiuka makubaliano hayo yaliyolenga kumaliza mzozo wa miezi minne kati ya pande hizo.

Kwa upande wake, Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu cha Iran (IRGC) kimesema vikosi vyake vya majini na anga vilifanya operesheni ya pamoja ya makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya vituo vya kijeshi vya Marekani nchini Kuwait na Bahrain, vikidai kuwa ilikuwa ni kulipiza kisasi kwa mashambulizi ya hivi karibuni yaliyofanywa na Marekani dhidi ya Iran.

Katika taarifa iliyonukuliwa na Press TV, IRGC imesema kuwa ukiukaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano unakwenda kinyume na Kifungu cha Kwanza cha Hati ya Makubaliano ya Islamabad na unaweza kusababisha kusitishwa kabisa kwa mchakato wa mazungumzo ya kidiplomasia.