
PAWAGA, iliyokuwa ikitajwa zaidi kama eneo la uzalishaji wa mpunga pekee, sasa imeanza kujijengea sifa mpya ya kuwa kitovu cha uchumi wa kilimo nchini baada ya uwekezaji mkubwa wa Serikali katika umwagiliaji, umeme, maghala ya kuhifadhi mazao na barabara kuchochea kuanzishwa kwa viwanda 17 vya kuchakata mpunga, kuongeza ajira kwa vijana na kuinua kipato cha maelfu ya wakulima.
Tofauti na miaka michache iliyopita ambapo wakulima walilazimika kuuza mpunga ghafi kwa bei ya hasara mara baada ya mavuno kutokana na ukosefu wa maghala na soko la uhakika, Pawaga imejenga mnyororo kamili wa thamani unaowawezesha wakulima kuchakata mazao yao, kuyahifadhi na kuyauza kwa thamani kubwa.
Mabadiliko hayo yalibainishwa na Mbunge wa Jimbo la Isimani, Emanuela Mtatifikolo Kaganda, alipotembelea Kiwanda cha Ndete Starch Q kilichopo Kijiji cha Itunundu, kinachochakata mpunga kwa kutumia teknolojia ya kisasa.

Amesema serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan imeweka mazingira yaliyowezesha sekta binafsi kuwekeza katika viwanda vya kuongeza thamani ya mazao, hatua inayochochea uchumi wa wananchi na kuongeza mapato ya Serikali.
“Miaka ya nyuma mkulima alikuwa analazimika kuuza mpunga mara tu baada ya kuvuna kwa sababu hakukuwa na maghala ya kuhifadhi. Leo anaweza kuhifadhi, kuchakata na kuuza mchele kwa bei nzuri zaidi. Haya ndiyo matokeo ya uwekezaji wa Serikali,” amesema Mtatifikolo.
Amesema kupitia mpango wa Big Results Now (BRN), Serikali imejenga maghala ya kuhifadhi mazao, huku umeme wa REA ukiwa kichocheo kikubwa cha kuanzishwa kwa viwanda vya uchakataji wa mpunga vinavyoongeza thamani ya mazao yanayolimwa Pawaga.

Kwa mujibu wa mbunge huyo, Tarafa ya Pawaga sasa ina viwanda 17 vya kuchakata mpunga, ambavyo mbali na kuwapa soko wakulima, vimezalisha ajira kwa mamia ya vijana katika uchakataji, upakiaji, usafirishaji na shughuli nyingine zinazozunguka sekta ya kilimo.
Amesema serikali inaendelea kuondoa vikwazo vya usafirishaji wa mazao kwa kuboresha mtandao wa barabara, ambapo tayari imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa kilomita 20 za barabara ya Pawaga kuelekea Iringa Mjini, zaidi ya Sh bilioni 1.2 kwa barabara ya Pawaga–Izazi na Sh milioni 800 katika bajeti ya mwaka huu kuendeleza mradi huo.
Aidha, amesema uwekezaji wa zaidi ya Sh Bilioni 56 katika Skimu ya Umwagiliaji ya Mkombozi utaongeza uzalishaji wa mpunga na mazao mengine ya biashara, hatua inayoiweka Pawaga katika nafasi nzuri ya kuchangia usalama wa chakula na ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Mkurugenzi wa Kiwanda cha Ndete Starch Q, Luka Ndete, alisema uwekezaji huo umeifanya Pawaga kuwa moja ya maeneo yanayokua kwa kasi katika uzalishaji wa mpunga na mazao ya bustani.
Amesema upatikanaji wa umeme wa uhakika umeongeza ufanisi wa viwanda, huku ujenzi wa barabara ya Pawaga–Izazi ukitarajiwa kupunguza gharama za usafirishaji na kufungua masoko makubwa zaidi, hususan Mkoa wa Dodoma.
Kwa mujibu wake, mafanikio hayo yameongeza pia uzalishaji wa vitunguu, nyanya na mboga mbalimbali, huku biashara za usafirishaji, pembejeo za kilimo, malazi na huduma nyingine zikikua sambamba na ongezeko la uzalishaji.
Naye Afisa Tarafa wa Pawaga, Emanuel Ngabuji, alisema uwekezaji uliofanywa na Serikali umeifanya Pawaga kuwa miongoni mwa maeneo yanayoongoza kwa uzalishaji wa mpunga nchini.
Amesema wakulima wengi sasa wanauza mchele uliokwishaongezewa thamani badala ya mpunga ghafi, hali inayoongeza kipato cha kaya na kuifanya tarafa hiyo kuwa kitovu muhimu cha biashara ya nafaka ndani na nje ya Mkoa wa Iringa.
Katika kuonyesha kuwa maendeleo yanapaswa kugusa pia maisha ya wananchi mmoja mmoja, Mtatifikolo alikabidhi mabati kwa waendesha bodaboda wa Kijiji cha Itunundu ili kuwawezesha kukamilisha ujenzi wa kijiwe chao.
Wakizungumza baada ya kupokea msaada huo, wawakilishi wa waendesha bodaboda walisema mabati hayo yatawasaidia kupata sehemu salama ya kufanyia shughuli zao za kila siku, kuboresha huduma kwa wateja na kuongeza kipato chao.
Ziara ya mbunge huyo imekuwa sehemu ya ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi, huku ikionyesha namna uwekezaji mkubwa wa Serikali katika miundombinu unavyoenda sambamba na hatua za kuwainua wananchi katika ngazi ya jamii.
0 Comments